Siku moja baada ya waasi hao kuingia katika mji wa Goma, waandamanaji walishambulia majengo ya Umoja wa Mataifa pamoja na balozi za Rwanda, Ufaransa na Marekani katika mji mkuu, Kinshasa, wakionyesha hasira kwa kile walichosema ni kuingiliwa na mataifa ya kigeni.
Waasi wa M23 waliingia mjini Goma siku ya Jumatatu katika kile kinachoelezwa kama zuzidi kwa kiasi kikubwa, kwa mzozo wa miongo mitatu. Walikuwa wakiendelea kukabiliana na upinzani kutoka kwa jeshi na wafuasi wao.
Siku ya Jumanne, mashambulizi ya kutumia silaha ndogo ndogo yaliendelea mitaani, ambapo maiti nyingi zilionekana, alisema Jens Laerke, msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kibinadamu (OCHA), akinukuu ripoti kutoka kwa wafanyikazi katika jiji hilo.
"Hali ya kibinadamu ndani na karibu na Goma bado inatia wasiwasi," Laerke aliuambia mkutano mjini Geneva, Uswizi.
"Hospitali za Goma zinaripotiwa kuzidiwa, zikijitahidi kudhibiti mmiminiko wa watu waliojeruhiwa," aliongeza. Alisema pia kuna ripoti za ubakaji unaofanywa na wapiganaji.
Forum