“Mapigano bado yanaendelea,” alisema Bruno Lemarquis, mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini DRC.
“Ni hali ya kutatanisha. Ni hali hatari sana.”
Aliwambia waandishi wa habari kupitia mahojiano ya video akiwa katika mji mkuu wa DRC, Kinshasa kwamba “ Mapigano makali yamekuwa yakiendelea katika mitaa yote” ya Goma huko Kivu Kaskazini.
Lemarquis alisema kumekuwa na tatizo kubwa la maji, umeme, intaneti na huduma ya simu. Maghala ya misaada ya kibinadamu yameporwa.
“Kwa niaba ya jumuia ya mashirika ya misaada ya kibanadamu, natoa wito kwa pande zote kukubaliana juu ya sitisho la muda la mapigano katika maeneo yanayoathirika zaidi na kutoa njia salama kuhakikisha shughuli za kutoa misaada zinaanza tena. Na muhimu zaidi, kurahisisha pia njia salama ili kuwaondoa watu waliojeruhiwa na raia waliobanwa katika maeneo ya mapigano,” Lemarquis aliongeza.
Umoja wa Mataifa Jumapili ulitangaza msaada wa dola milioni 17 kutoka kwenye mfuko wake wa dharura kwa ajili ya mahitaji muhimu ya kibinadamu nchini DRC.
Hayo yakiarifiwa, mapigano ya wapiganaji wa M23 na jeshi la Congo mjini Goma, yameua takriban watu 17 na kujeruhi wengine 367, kulingana na takwimu za hospitali kadhaa ambazo zimeonwa na shirika la habari la AFP.
Forum