Akitaja juu ya kuongezeka kwa ripoti za kuaminika za mateso na ukiukaji wa haki za binadam Blinken aliihimiza serikali ya Ethiopia kuchukua hatua za mara moja kuwalinda raia wake pamoja na wakimbizi na kuzuia ghasia zaidi kutokea.
Waziri Blinken ameiomba serikali ya Addis Ababa kusitisha uhasama mara moja na kuondolewa kwa wanajeshi huko Tigray pamoja na jimbo la Amhara, na kuondolewa kwa wanajeshi wa Eritrea.
Aliiomba serikali pia kufanya kazi na Jumuia ya Kimataifa ili kurahisisha uchunguzi huru wa kimataifa katika tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu na kuwa wajibisha wahusika.
Ripoti ya ndani ya serikali ya Marekani ambayo gazeti la The New York Times imeipata inasema kuwa Ethiopia inaendesha “kampeni maalum ya kutokomeza kabila moja”.
Kampeni hiyo inafanyika kwa kisingizio cha vita katika mkoa wa Tigray, eneo ambalo kwa kiasi kikubwa linadhibitiwa na wanamgambo wa Amhara upande wa kaskazini mwa nchi.
Gazeti laThe Times lilieleza kuwa ripoti hiyo, iliyoandikwa mapema Februari, inafafanua “waziwazi ardhi inayoshuhudia nyumba zilizovamiwa na kuibiwa thamani zake na vijiji vilivyotelekezwa ambapo maelfu ya watu hawajulikani walipo.”
Kulingana na ripoti hiyo imegundua kuwa maafisa wa Ethiopia na wapiganaji ambao ni washirika wao kutoka mkoa jirani wa Amhara, ambao walihamia Tigray kumsaidia Waziri Mkuu Abiy Ahmed, wanafanya “kwa makusudi na ufanisi mpango wa kuhamisha kabila mmoja la Tigray Magharibi kwa kutumia nguvu na manyanyaso.”