Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 04:20

Polisi Ethiopia waendelea kumshikilia mwandishi wa Reuters


Mwanahabari Kumerra Gemechu
Mwanahabari Kumerra Gemechu

Mwanahabari mpiga picha wa shirika la habari la Reuters Kumerra Gemechu, alikamatwa na polisi wa Ethiopia mjini Addis Ababa tangu Alhamisi na ataendelea kuzuiliwa kwa angalau wiki mbili zijazo, familia yake imesema Jumatatu.

Familia inasema mwanahabari huyo bado hajafunguliwa mashtaka na pia haikuelezwa sababu za kukamatwa kwake, na kufikia sasa polisi haijajibu maombi ya Reuters kuhusu sababu za kukamatwa mwanahabari wake.

Kumerra mwenye umri wa miaka 38, amefanya kazi na Reuters kama mpiga picha wa kujitegemea kwa miaka 10.

Katika kesi iliyosikilizwa kwa muda mfupi siku ya ijumaa, bila wakili kuwepo mahakamani, jaji aliamuru Kumerra aendelee kushikiliwa kwa siku nyingine 14 ili polisi ipate muda zaidi wa kuendelea na uchunguzi wake, familia ya mwanahari huyo imesema.

Katika taarifa yake Jumatatu, Reuters limelaani vikali kuzuiliwa kwa Kumerra. Mwanahabari huyo amekamatwa baada ya mwanahabari mwengine mpiga picha wa Reuters, Tiksa Negeri, kupigwa na maafisa wawili wa polisi tarehe 16 Disemba.

“Kumerra ni sehemu ya timu ya Reuters ambae anaripoti kutoka Ethiopia kwa njia ya haki, huru na isiyoegemea upande wowote. Kazi ya Kumerra imeonyesha weledi wake , na hatujui msingi wa kumuweka kizuizini”, mhariri mkuu wa Reuters Stephen Adler amesema katika taarifa.

“Lazima wanahabari waruhusiwe kuripoti habari kwa faida ya umma bila kuwa na wasiwasi wa kunyanyaswa au kuhujumiwa, mahali popote walipo. Hatutapumzika hadi Kumerra ameachiwa huru”, Adler ameongeza.

Kumerra amekua akiripoti kuhusu mzozo wa jimbo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia, lakini Reuters haiwezi kuhakikisha kwamba kukamatwa kwake kuna uhusiano na kazi yake.

XS
SM
MD
LG