Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 04:25

UNHCR inarudia wito kwa serikali ya Ethiopia kuwapatia fursa ya kuwafikia wakimbizi


Asafu Alamaya, ana miaka 80 raia wa Ethiopia alikimbia mapigano kwenye mkoa wa Tigray Disemba 2020
Asafu Alamaya, ana miaka 80 raia wa Ethiopia alikimbia mapigano kwenye mkoa wa Tigray Disemba 2020

UNHCR inakadiria wakimbizi 15,000 hadi 20,000 walikimbia kwenye kambi mbili za kaskazini na wametawanyika katika maeneo ambayo hakuna uwezo wa kuyafikia. Shirika hilo linasema wengi wapo katika hatari kubwa na wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi wa kuokoa maisha yao

Shirika la kuwahudumia wakimbizi katika Umoja wa Mataifa linaonya kwamba maelfu ya wakimbizi wa Eritrea huko kaskazini mwa Ethiopia katika mkoa wa Tigray uliokumbwa na mzozo wanahitaji msaada na ulinzi. Shirika hilo linarudia tena wito wake kwa serikai kutoa fursa kuwafikia wakimbizi.

Kabla ya kuanza mashambulizi ya jeshi la Ethiopia huko Tigrey mwanzoni mwa Novemba mwaka jana, shirika hilo la kuhudumia wakimbizi katika Umoja wa Mataifa liliwahudumia wakimbizi takribani 96,000 wa Eritrea katika kambi nne. Tangu wakati huo shirika hilo limepoteza udhibiti kwenye kambi na uwezo wake wa kutoa misaada muhimu kwa wakimbizi.

Tangu mwanzoni mwa Januari, Ethiopia imetoa fursa kwa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kibinafsi kufika katika kambi mbili huko kusini mwa Tigray. Program ya chakula Duniani inaripoti kwamba imefanikiwa kuwapatia wakaazi 26,000 waliopo kwenye kambi mgao wa dharura wa chakula na lishe, lakini linasema msaada zaidi wa chakula na huduma nyingine unahitajika.

Hali kwa ujumla ni mbaya kwa wakimbizi huko kaskazini mwa Tigray. Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema kambi mbili zilijikuta katikati ya majibizano ya risasi kwenye mzozo uliosababisha uharibifu mkubwa sana wa miundo mbinu. Maelfu ya wakimbizi wa Eritrea walikimbia kwa ajili ya usalama wao kutoka kwenye kambi hizo.

Babar Baloch, msemaji wa UNHCR
Babar Baloch, msemaji wa UNHCR

Msemaji wa UNHCR, Babar Baloch anasema wa-Eritrea wapatao 4,000 walielekea kambi ya Mai Aini huko kusini mwa Tigray, Anasema mkuu wa shirika la wakimbizi katika Umoja wa Mataifa, Filippo Grandi amekutana na baadhi ya wakimbizi hao kwenye ziara yake kwenye kambi mwanzoni mwa wiki iliyopita. Baloch anasema wakimbizi walimwambia kamishna mkuu kuhusu uzoefu wao unaowapa kiwewe na hofu ya baadae.

“Baadhi walisema walikuwa wameamua kula majani kwasababu hakuna chakula kingine chochote. Walizungumzia pia juu ya kupenya kwa wahusika wenye silaha katika kambi, kuwepo mauaji, utekaji na pia wengine walilazimishwa kurudi Eritrea mikononi mwa vikosi vya Wa-Eritrea waliopo katika eneo hilo”

UNHCR inakadiria wakimbizi 15,000 hadi 20,000 walikimbia kwenye kambi mbili za kaskazini na wametawanyika katika maeneo ambayo hakuna uwezo wa kuyafikia. Shirika hilo linasema wengi wapo katika hatari kubwa na wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi wa kuokoa maisha. Inasema fursa kamili ya kufika huko lazima itolewe hivi sasa kwa mashirika ya misaada ili kuzuia hali ambayo tayari ni mbaya kuwa mbaya zaidi.

Ripoti ya karibuni kutoka ofisi ya UN inayoratibu masuala ya ndani ya kibinadamu inaonya juu ya janga linalokuja la kibinadamu. Inakadiria zaidi ya watu milioni 2.3 kwenye mkoa wote wa Tigray uliokumbwa na mzozo wanahitaji msaada wa haraka wa kuokoa maisha yao.

XS
SM
MD
LG