Mwaka 2013, Tanzania ilisaini muundo wa mkataba na kampuni ya China Merchant Holdings International, mwendeshaji mkubwa kuliko wote wa bandari ya China, kujenga bandari na zoni maalum ya kibiashara ambayo inalengo la kuibadilisha nchi hiyo ya Afrika Mashariki kuwa ni kituo cha biashara cha kieneo na usafirishaji.
Jiwe la msingi la ujenzi wa bandari hiyo liliwekwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete mwaka 2015 na ulitarajiwa kugharimu dola za Marekani bilioni 10.
Vyanzo vya habari vimesema kuwa kama Bandari hiyo ingejengwa ingekuwa kubwa zaidi Afrika Mashariki ikiwa na ekari 3,000 na viwanda 190.
Akizungumza Ijumaa kwenye mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) uliowashirikisha wafanyabishara kutoka wilaya 139 nchini, Rais Magufuli alisema “kwenye mkataba wa ujenzi wa bandari hiyo kulikuwa na vipengele vya ovyo”.
Alisema moja ya masharti hayo ni kutojengwa wala kuendelezwa kwa bandari yoyote kuanzia eneo la Tanga hadi Mtwara.
“Yaani kwenye eneo lote kuanzia Tanga hadi Mtwara kusijengwe bandari yoyote. Bandari ya Kilwa tusiiendeleze, Bandari ya Mtwara ambayo itawezesha mikoa ya kusini kupokea mafuta badala yake Dar es Salaam kisha yarudi huko, hatutakiwi kuiendeleza, Barabara kutoka Mtwara hadi Bamba Bay ambayo itatuwezesha kusafirisha mizigo hadi Msumbiji tusiijenge," alisema Rais Magufuli.
Alisema sharti jingine ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutotakiwa kwenda kukusanya ushuru wala kodi katika eneo lile na walitaka wapewe hakikisho la miaka 33.
Pia alisema wawekezaji hao wangeweza kumiliki ardhi kwa hati ya miaka 99 pamoja na kutoruhusiwa kuulizwa nani anamiliki eneo hilo.
Rais Magufuli alisema sharti lingine ni gharama zitakazotumiwa na mwekezaji huyo katika ujenzi wa bandari hiyo zinatakiwa zirejeshwe.
Kutokana na kutokubaliana na masharti hayo, serikali ya Tanzania imewaandikia rasmi waendeshaji wa bandari ya China juu ya kupinga masharti hayo, Deusdedit Kakoko, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Tanzania aliliambia shirika la habari la Uingereza Reuters hivi karibuni.
“Tunasubiri waanze mazungumzo mapya. Wakati wakiwa tayari, sisi tutaanza mazungumzo.”