Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 04:10

DRC: M23 wachukua udhibiti wa mji muhimu kimkakati wa Kanyabayonga


Waasi wa kundi la M23 wakilinda eneo hilo wakati wa mkutano kati ya maafisa wa Kikosi cha Afrika Mashariki (EACRF) na waasi wa M23 katika kambi ya Rumangabo huko DRC Januari 6, 2023. Picha na Guerchom Ndebo/AFP
Waasi wa kundi la M23 wakilinda eneo hilo wakati wa mkutano kati ya maafisa wa Kikosi cha Afrika Mashariki (EACRF) na waasi wa M23 katika kambi ya Rumangabo huko DRC Januari 6, 2023. Picha na Guerchom Ndebo/AFP

Wapiganaji wa M23 wanaoaminika kuungwa mkono na Rwanda wameuteka mji wa kimkakati mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, afisa mmoja aliliambia shirika la habari la AFP Jumamosi, huku maeneo jirani pia yakiangukia mikononi mwa waasi.

Mji wa Kanyabayonga upo upande wa kaskazini katika jimbo la Kivu Kaskazini, ambalo limekumbwa na ghasia tangu 2021 wakati M23 (March 23 Movement) ilipoanzisha tena mashambulizi ya kutumia silaha katika eneo hilo.

Mji huo una watu zaidi ya 60,000 na darzani za maelfu yao wamekimbilia huko katika miezi ya hivi karibuni, wakifukuzwa kutoka kwa makazi yao na waasi.

"Kanyabayonga imekuwa mikononi mwa M23 tangu Ijumaa jioni," afisa wa utawala wa eneo hilo alisema kwa sharti la kutotajwa jina.

Mji huo unachukuliwa kuwa njia muhimu ya kuelekea Butembo na Beni kaskazini, ngome za kabila la Nande na vituo vikuu vya kibiashara.

Mji huo uko katika eneo la Lubero, eneo la nne kwa ukubwa katika jimbo la Kivu Kaskazini ambalo kundi hilo limeingia baada ya Rutshuru, Nyiragongo na Masisi.

Afisa huyo wa utawala alisema kuwa wakazi wa Kanyabayonga "hawana mahali popote pa kwenda, ni ukiwa kabisa, watu imechoka".

"Tunaona mmiminiko wa watu waliokimbia makazi yao kutoka Miriki, Kirumba na Luofu kuelekea Kaskazini," msimamizi wa kijeshi wa eneo la Lubero Kanali Alain Kiwewa alisema.

"Ni hali inayotutia wasiwasi," aliongeza. Miji mingine ya karibu imetekwa na M23, kulingana na maafisa na vyanzo vya usalama.

M23 wameudhibiti mji uitwao Kanya takriban kilomita 17 (maili 10) kaskazini mwa Kanyabayonga, afisa wa utawala aliiambia AFP Jumamosi, akiongeza kuwa mtu mmoja aliuawa kwa kugongwa na risasi ndani ya nyumba yake..

Mwandishi mmoja wa habari ameliambia shirika la habari la AFP kwamba ameona maiti nne katika mji huo, wanajeshi wawili na raia wawili, ingawa kiongozi wa vijana katika mji huo alielezea hali kuwa shwari "kwa sasa".

Wakati wa mkutano siku ya Jumamosi waasi waliwaambia wakazi wa Kayna kwamba walikuwa wamekuja katika mji huo kuwahakikishia usalama, kiongozi mmoja wa mashirika ya kiraia alisema.

Kayna ilishuhudia mapigano usiku kucha, huku kiongozi wa vijana akisema kwamba wale waliokimbilia mjini kutoka Kanyabayonga "walilala nje usiku".

Risasi zilisikika usiku kucha,” alisema. "Hatujui tena tumgeukie nani." Kijiji cha Luofu, ambacho kiko umbali wa kilomita 18 kutoka Kanyabayonga, pia kimedhibitiwa na waasi.

"Luofu tangu saa tatu asubuhi imekuwa chini ya udhibiti wa M23," chanzo cha usalama ambacho hakikutaka kutajwa jina kiliiambia AFP kwa njia ya simu, na kuongeza kuwa kuna zaidi ya kaya 5,000 huko.

Huko Kirumba, takriban kilomita 25 kutoka Kanyabayonga, idadi ya watu iko katika "hali ya hofu", kiongozi mmoja wa mashirika ya kiraia alisema kwa sharti la kutotajwa jina.

"Hatuwezi kuhama tena, tutaenda wapi? Hatujui pa kwenda," alisema. Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, eneo lenye utajiri wa madini limekuwa likishuhudia ghasia kwa miaka 30 zikitekelezwa na makundi yenye silaha, ya ndani na nje ya nchi, ambayo yalityokana na vita vya kikanda vya miaka ya 1990.

Rwanda inakanusha kuwa inaunga mkono M23. Ofisi ya Pamoja ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema katika ripoti yake ya kila mwezi Ijumaa kwamba mapigano katika eneo hilo yanasababisha raia wengi kuyahama makazi yao.

"Mashirika ya kibinadamu yanayotoa msaada kwa waliohamishwa yamesitisha shughuli zao kwa sababu za kiusalama," ilisema.

Forum

XS
SM
MD
LG