Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 04:32

Siku ya Mkimbizi: Idadi ya Wakimbizi duniani yafikia milioni 120 mpaka sasa.


The Inside Story - World Refugee Day THUMBNAIL skinny
The Inside Story - World Refugee Day THUMBNAIL skinny

Dunia leo inaadhimisha siku ya wakimbizi, kauli mbiu ikiwa ni “mshikamano na wakimbizi.”

Dunia leo inaadhimisha siku ya wakimbizi, kauli mbiu ikiwa ni “mshikamano na wakimbizi.”

Serekali, mashirika mbalimbali ya kiserekali na binafsi duniani kote huungana na shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR katika dhima ya kuangazia hali za watu wanaokimbia mataifa yao kwa sababu ya matatizo mbalimbali.

Migogoro inayosababisha vita imekuwa chanzo kikubwa cha kuzalisha wakimbizi na kujikuta katika kambi ndani na nje ya mataifa yao.

Baadhi yao wanaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali za hali zao za ukimbizi.

Miaka minne iliyopita, Erken Ndamumvirubisa, mkimbizi kutoka Burundi alizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika katika kambi ya Nduta, Kigoma, Tanzania.

Alielezea adha yake kubwa ya kuishi kambini kuwa ni hali mbaya ya kiuchumi inayomkabili ili kuendesha maisha yake.

“Uchumi hapa kambini, hasa biashara haiendi kwa sababu hatuna soko la muungano ambalo linatuwezesha kufikisha mahitaji kama kubadilishana chakula. Siku zilizopita tulikuwa na soko la muungano, kama ukipeleka njegere wanakupa maharage, ukipeleka unga wanakupa muhogo lakini soko kwa sasa hatuna. Tunatamani tuwe na soko la kufanya biashara ili kujipatia fedha za mahitaji.”

Ndamumvirubisha, anazungumzia moja ya changamoto ambayo wakimbizi wanakabiliana nayo kambini, lakini si Nduta tu, bali hata kuanzia Sudan, Gaza, Myanmar mpaka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kwa mujibu wa ripoti ya hali ya mwenendo wa wakimbizi duniani ya mwaka 2024 yaani “2024 Flagship Global Trends Report,” ya UNHCR, kiwango cha ongezeko la wakimbizi kimefikia kiwango cha kihistoria.

Kwa mwaka jana mpaka 2024 migogoro inayoendelea katika maeneo mbalimbali duniani kote imefanya hali kuwa mbaya.

Mpaka mwezi mei 2024, dunia imeshuhudia ongezeko la watu milioni 120 waliolazimishwa kukimbia makazi yao, ikiwa ni ongezeko la 12 mfululizo kwa kila mwaka ripoti ya UNHCR inaeleza.

Amin Ally, ni mchambuzi wa masuala ya siasa na migogoro kutoka Seattle, Washington State, Marekani, anasema hali hii itazidi kuongezeka endapo migogoro haitamalizwa.

"Kama migogoro itaendelea kuongezeka kama ilivyo sasa idadi ya wakimbizi itaongezeka. Tunashuhudia mizozo kuanzia Gaza, Sudan, DRC, na hata wahamiaji kutoka Amerika Kusini wanaotaka kuingia Marekani, kwa sababu mbalimbali. Kama haya hayata shughulikiwa badi hali hii itazidi."

Sababu kubwa ya ongezeko maradufu la wakimbizi, UNHCR inasema ni mgogoro wa Sudan ambao umechangia raia milioni 10.8 kuwa wakimbizi mpaka mwishoni mwa 2023.

Katika mataifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na Myanmar, mamilioni walikimbia makazi yao kwa mapigano ambapo inakadiriwa mpaka mwishoni mwa mwaka jana hadi watu milioni 1.7, sawa na asilimia 75 ya idadi ya watu wa mataifa hayo waligeuka kuwa wakimbizi.

Vita vibaya vya Ukanda wa Gaza vimeongeza wakimbizi wa Palestina, na Syria na kufikia milioni 13.8.

Tanzania inaanza kufanya tathimini ya wakimbizi wa burundi wanaostahili kubaki kambini au kurejea nyumbani.

Kwa muda kumekuwa na mvutano kati ya wakimbizi na serekali ya Tanzania, ikidaiwa kulazimishwa kurejea Burundi kwa vile hali ni shwari.

Hata hivyo Tanzania, imekanusha hilo na kudai waliorejea walifanya hivyo kwa hiari yao.

Ripoti ya UNHCR inaonyesha duniani kote zaidi ya wakimbizi milioni moja walirejea makwao mwaka jana.

Amin Ally anasema Serekali ya Tanzania, wakimbizi wa Burundi, na shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR, wote wana hoja juu ya mvutano wa wakimbizi wa Burundi, Tanzania.

"Wakimbizi wanasimamiwa na sheria za kimataifa. Ili uwe mkimbizi lazima utokako kuwe na matatizo, na pakitulia basi urejee. Kwa sasa hali ya Burundi ikoje? Kama kuna utulivu kwa kufuata sheria za kimataifa, inapoonekana kuna usalama watarudi, lakini pia Burundi iwahakikishie usalama wao"

Uganda ni miongoni mwa mataifa yanayopokea wakimbizi wengi. Kwa muda mrefu imekuwa ikipokea wakimbizi kutoka mataifa ya DRC, na Sudan Kusini, lakini sana Sudan nayo imeongezeka.

Uganda inaruhusu wakimbizi kuishi katika jamii na si kambini pekee.

Inakadiriwa Wasudan 40,000 waliwasili Uganda katika miezi ya karibuni lakini changamoto kubwa kwao ni lugha ya Kiingereza.

Halima Athumani mwandishi wa VOA Uganda, katika ripoti yake wakimbizi wa Sudan wanasema lugha ni changamoto kwao.

Razan Abdulrahim Muhammad alikimbia Sudan mwezi Machi na kupoteza mawasiliano na mumewe. Sasa anajifunza kingereza ili apate ajira Uganda.

“Ninataka kuwa vizuri ili niweze kuomba kazi na kuhudumia watoto wangu.”

Vita vya mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo vimewaathiri pia hadi baadhi ya wanahabari wa maeneo mbalimbali na kuwalazimisha kuwa wakimbizi.

Ismael Matungulu ni mmoja wa wanahabari saba wanaoishi kambini Mugunga Lushagala baada ya kukumbia mji wa Sake ambako alikuwa na kituo chake cha Radio SAKE FM, baada ya mapigano ya kundi la M23.

“Ndio, kwa kweli tunapatikana hapa ndani ya kambi ya wakimbizi ya Lushagala kwasabu ya ukosefu wa usalama katika wilaya ya Masisi hasa katika Mji wa sake na leo tunapitia maisha magumu hali ambayo ni mbaya sana.”

Ikiwa maadhimisho ya mwaka huu yanaangazia mshikamano na wakimbizi, UNHCR inasema changamoto kubwa imekuwa ni katika kutekeleza hilo.

Sheria na sera za mataifa yanayopokea wakimbizi zimekuwa na utofauti na kuleta changamoto katika kufanikisha malengo ya kuwafanya wakimbizi wawe sehemu ya jamii nje ya mataifa yao.

Dkt Timothy Sadera, anashughulika na wakimbizi pamoja na wahamiaji katika jiji la Atlanta, Georgia, Marekani. Ansema mshikamano na wakimbizi inawezekana japo kuna changamoto.

"Hilo linawezekana japo kuna changamoto. Wakimbizi wanatoka sehemu tofauti, na inapaswa kuzowea mazingira mapya. Lakini kuna seheria na sera za nchi walizo kimbilia ambazo zitaamua kwa namna gani wanaweza kuchangamana."

Swali kubwa linabaki kuwa je, tutarajie ongezeko ama kupungua kwa watu milioni 120 ambao kwa sasa wanaishi na hadhi ya ukimbizi duniani kote?

Taarifa hii imeandaliwa na Idd Ligongo.

Forum

XS
SM
MD
LG