Afisa wa usalama mashariki mwa nchi ameliambia shirika la habari la AFP kwa masharti ya kutotajwa jina kwamba mkandarasi wa kijeshi wa kibinafsi aliuawa, na wengine watatu kujeruhiwa siku ya Jumamosi katika shambulio la kombora dhidi ya kambi ya jeshi la Congo karibu kilomita 10 kaskazini mwa mji wa Goma.
Mji mkuu huo wa Kivu Kaskazini umezingirwa katika eneo la kaskazini na magharibi na waasi wa M23.
Mapigano dhidi ya jeshi la Congo hufanyika mara kwa mara katika vitongoji vya mji huo, wakati waasi wanaendelea kuimarisha udhibiti wao mashariki mwa nchi.
Wizara ya Romania ya mambo ya nje Jumapili ilisema kwamba mtu aliyeuawa na wawili waliojeruhiwa ni raia wa Romania, na kwamba mtu wa nne aliyejeruhiwa ni raia wa nchi nyingine.
Vituo kadhaa vya televisheni vya Romania, zikiwemo televisheni mbili zinazomilikiwa na serikali, zilimuelezea mpiganaji aliyeuawa kama “mamluki wa Romania” chini ya mkataba na jeshi la Congo.
Kwenye umbali wa kilomita 200 kaskazini mwa Goma, huko Butembo, wanajeshi wawili walijeruhiwa katika shambulio la kuvizia, kiongozi wa eneo hilo Kanali Alain Kiwewa ameiambia AFP.
Forum