Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 01:09

Korea Kaskazini yafunga ubalozi wake wa muda mrefu Uganda


Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un akimkaribisha Makamu wa zamani wa Rais wa Uganda Edward Kiwanuka Ssekand alipokwenda Pyongyang. Picha na KNS / KCNA / AFP.
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-Un akimkaribisha Makamu wa zamani wa Rais wa Uganda Edward Kiwanuka Ssekand alipokwenda Pyongyang. Picha na KNS / KCNA / AFP.

Korea Kaskazini inafunga ubalozi wake nchini Uganda, maafisa walisema, ukimaliza uwepo wa kidiplomasia wa nusu karne katika mojawapo ya washirika wake wa muda mrefu zaidi wa Afrika.

Hatua hiyo imetangazwa baada ya mkutano wa Jumatatu kati ya Rais wa Uganda Yoweri Museveni na balozi wa Korea Kaskazini Jong Tong Hak.

"Balozi Jong alimweleza rais kwamba Korea Kaskazini imechukua hatua ya kimkakati kupunguza idadi ya balozi zake barani Afrika, ikiwa ni pamoja na Uganda, ili kuongeza ufanisi wa taasisi za nje ya nchi," ilisema taarifa ya rais wa Uganda ambayo shirika la habari la AFP iliipata.

"Urafiki wetu mzuri utaendelea na utaimarishwa na kuendelezwa zaidi," Jong alinukuliwa akisema, akiongeza kuwa uhusiano wa kidiplomasia kwa sasa utafanyika kupitia ubalozi wake ulioko Malabo, Equatorial Guinea.

Korea Kaskazini ilianzisha uhusiano na Uganda muda mfupi baada ya kupata uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1962, na kumuunga mkono Idi Amin aliponyakua mamlaka mwaka 1971, ikitoa mafunzo na silaha kwa majeshi yake.

Ilifungua ubalozi huo mjini Kampala mwaka mmoja baadaye wakati jumuiya ya kimataifa ikimtenga Amin, ambaye utawala wake wa kikatili ulidumu hadi mwaka 1979.

Baada ya Museveni kuchukua madaraka mwaka 1986, Kampala na Pyongyang zilitia saini mikataba ya ushirikiano ambayo iliishuhudia Korea Kaskazini ikiipatia nchi hiyo ya Afrika Mashariki silaha na zana nyingine za kijeshi pamoja na kutoa mafunzo kwa vikosi vyake vya usalama.

Lakini Mei 2016, Uganda ilisema inasitisha ushirikiano wa kijeshi na Pyongyang baada ya Umoja wa Mataifa kuiwekea Pyongyang vikwazo vizito kutokana na mpango wake wa nyuklia.

Museveni alifanya ziara kadhaa nchini Korea Kaskazini, ambako alikutana na kiongozi wa nchi hiyo marehemu Kim Jong Il, baba yake kiongozi wa sasa Kim Jong Un.
Chanzo cha habari hii ni Shirika la habari la AFP

Forum

XS
SM
MD
LG