Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 23:10

Waasi wameshambulia wanajeshi wa Uganda mashariki mwa DRC


Wanajeshi wa Uganda wakiwa wanashika doria mashariki mwa DRC
Wanajeshi wa Uganda wakiwa wanashika doria mashariki mwa DRC

Wanajeshi wawili wa Uganda wamelazwa hospitalini wakiwa katika hali mahtuti baada ya kupigwa risasi na kundi la waasi masahriki mwa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Msafara wa wanajeshi wa Uganda UPDF, ulishambuliwa ukiwa kwenye barabara ya kutoka Bunagana kuelekea Rutshuru.

Msemaji wa jeshi la Uganda Brig Felix Kulaigye amethibitisha tukio hilo.

“Ni kweli, wanajeshi wetu wawili wamepigwa risasi kichwani na waasi mashariki mwa DRC,” amesema Kulaigye, akiongezea kwamba “wamelazwa hospitalini wakiwa katika hali mbaya sana. Risasi zimekwama kichwani.”

Jeshi la Uganda linachunguza kundi la waasi lililohusika na shambulizi hilo.

Sehemu ambayo wanajeshi wa Uganda wanashika doria ipo karibu na sehemu kulipo wapiganaji wa kundi la waasi la M23, katika maeneo ya Bunagana, Rutshuru na Kiwanja.

Hata hivyo, Kulaigye amefutilia mbali madai kwamba huenda ni wapiganaji wa kundi la M23 walioshambulia msafara wa UPDF katika tukio hilo la Jumatatu asubuhi.

Mapigano makali

Viongozi wa jumuiya ya Afrika mashariki walikubaliana kutuma jeshi la pamoja EACRF kusaidia katika kuleta Amani mashariki mwa DRC, ikiwemo kuwapokonya silaha wapiganaji huku mazungumzo ya kisiasa yakiendelea.

Wanajeshi wanatoka Kenya, Uganda, Burundi na Sudan kusini.

Waasi wa M23 waliondoka katika sehemu walizokuwa wanashikilia na kuziachilia kwa jeshi la jumuiya ya Afrika mashariki.

Hata hivyo, serikali ya DRC imesisitiza kwamba kundi la M23 limeshikilia tena sehemu ambazo lilikuwa linadhibithi kabla ya jeshi la jumuiya ya Afrika mashariki kuwasili DRC.

Kulaigye amesema kwamba “wanajeshi wa Uganda walijibu shambulizi hilo haraka iwezekanavyo na wapiganaji waliokuwa wamejificha kwenye migomba ya ndizi, wafuatao 6, wakatoroka.”

Kulaigye amesisitiza kwamba “Tukishambuliwa, na sisi tutashambulia. Tuna uwezo wa kukabiliana vilivyo na yeyote atakayetushambulia. Wasijaribu tena kutushambulia.”

Makundi ya waasi yanayoungwa mkono

Vyanzo vya habari katika jeshi la Uganda vinasema kwamba wanafanya kazi katika eneo lenye makundi tofauti ya waasi yanayoaminika kuungwa mkono na serikali tofauti.

Serikali ya DRC inaamini kwamba waasi wa M23 wanaungwa mkono na serikali ya Rwanda. Serikali ya Rwanda nayo inaamini kwamba waasi wa FDLR wanaungwa mkono na serikali ya DRC. Kundi la waasi la Wazalendo vile vile linaungwa mkono na serikali ya DRC.

“Fighting M23 ni hatua inayoweza kutuweka katika mazingira magumu na serikali ya Rwanda. Kushambulia waasi wa Wazalendo, wanaungwa mkono na Kinshasa inatuweka katika mazingira magumu na serikali ya DRC ambayo inaunga Uganda mkono katika oparesheni ya Shujaa, dhidi ya waasi wa ADF,” amesema afisa wa UPDF ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Waasi wa Wazalendo walipigana na waasi wa M23 wiki iliyopita na kuwafurusha katika eneo la Kitchanga. https://www.voaswahili.com/a/wanamgambo-watiifu-kwa-serikali-ya-drc-wakomboa-mji-wa-kitshanga-kutoka-wa-waasi-wa-m23/7313100.html

Forum

XS
SM
MD
LG