Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 23:10

DRC: Mapigano makali Kitchanga, M23 wasisitiza kujilinda kwa kila hali


Wanajeshi wa Burundi walipowasili katika uwanja wa Goma, DRC, March 5, 2023 kuisaidia nchi hiyo kupata amani.
Wanajeshi wa Burundi walipowasili katika uwanja wa Goma, DRC, March 5, 2023 kuisaidia nchi hiyo kupata amani.

Mapigano makali yanaendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kati ya kundi lenye silaha linalojiita Wazalendo, ambalo linaungwa mkono na serikali na kundi la M23.

Jeshi la serikali likisaidiwa na wazalendo, wameudhibithi mji wa Kitchanga, Rutshuru, Kivu Kaskazini.

Mji huo ambao unaunganisha sehemu hiyo na mji wa Goma, ulidhibitiwa Jumatatu asubuhi baada ya mapigano makali kati ya wazalendo na waasi wa M23.

Makamanda wa kundi la wazalendo waliingia katikati ya mji wakisherehekea ushindi.

Msemaji wa kundi la M23 Lawrence Kanyuka, ametuma taarifa kwa vyombo vya habari leo Jumanne, akisema kwamba wana uhakika kwamba jeshi la DRC FARDC limeizingira Kitchanga kwa ushirikiano na jeshi la Burundi (BNDF).

Hatua hiyo “inavuruga kabisa maamuzi ya viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliyofikiwa katika kikao cha 20 kilichofanyika Bujumbura mnamo Februari 4, 2023,” amesema msemaji wa M23.

Waasi wa M23 walichukua udhibithi wa mji wa Kitchanga kutoka kwa wanajeshi wa serikali mnamo Februari 2023.

Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki waliiomba M23 kuuachilia mji wa Kitchanga kwa wanajeshi wa Burundi.

Shutuma dhidi ya jeshi la Burundi

Waasi wa M23 wamekuwa wakishutumu wanajeshi wa Burundi kwa kushirikiana na jeshi la Congo na kuachilia mji huo kwa serikali.

Burundi ilitoa taarifa wiki iliyopita, ikikanusha madai hayo.

Utawala wa rais Felix Tshisekedi umesisitiza kwamba jeshi lake halijafanya mashambulizi yoyote katika miezi ya hivi karibuni, na kwamba ni makundi huru ya wapiganaji yanayopigana na waasi wa M23.

Katika taarifa, kundi la M23 limesema kwamba lina haki ya kujilinda.

“Serikali ya DRC inastahili kuwajibika kwa uhalifu dhidi ya binadamu. M23 tuna haki ya kujilinda na kulinda maisha na mali za raia.”

Mji wa Kitchanga una jumla ya watu 60,000. Mji huo ulikuwa kambi kuu ya aliyekuwa kiongozi a waasi Laurent Nkunda.

DRC inataka wanajeshi wa EAC kuondoka Desemba 2023

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesema kwamba haitaongeza muda wa wanajeshi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaoshika doria mashariki mwa nchi hiyo.

Muda wa kikosi hicho cha wanajeshi kutoka Kenya, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo unakamilika Desemba 8 2023.

Naibu wa shughuli za kijeshi na ujasusi katika jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Meja Jenerali Tchaligonza Jacques, amesema kwamba wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki watatakiwa kuondoka DRC, wakati wa mkutano wa wakuu wa majeshi kutoka Afrika Mashariki, uliofanyika Addis Ababa, Ehiopia, Ijumaa wiki iliyopita.

Mkutano huo ulikuwa wa kujadiliana hali ya usalama inayoendelea kudorora mashariki mwa DRC ambapo wanajeshi wa serikali wanakabiliana na waasi wa kundi la M23. Serikali ya Rwanda imeripotiwa kuliunga mkono kundi la M23. Rwanda imekanusha ripoti hizo. Serikali ya Rwanda inadai kwamba DRC inawaunga mkono waasi wa FDLR wenye lengo la kuuangusha utawala wa Kigali. DRC imekanusha madai hayo.

Tshisekedi anataka walinda usalama wa MONUSCO kuondoka

Rais wa DRC Felix Tshisekedi, ambaye ametangaza kutetea muhula mwingine madarakani katika uchaguzi wa Desemba mwaka huu, amelikosoa sana jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushindwa kupigana na waasi wa M23.

Tshisekedi ametaka walinda usalama wa Umoja wa Mataifa MONUSCO, pamoja na wanajeshi wote wa kigeni kuondoka nchini humo.

Utawala wa Tshisekedi ulikuwa umeagiza wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuondoka nchini DRC mapema mwaka huu, lakini viongozi wa jumuiya hiyo wakamtaka Tshisekedi kuzingatia sana agizo lake na kuwa makini na hali ya usalama mashariki mwa DRC.

Kikao cha viongozi wa jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika Septemba 5, 2023, kilimtaka Tshisekedi kuongeza muda wa kikosi cha jeshi la jumuiya hiyo hadi Desemba 8 2023.

Mapiganao yameanza tena mashariki mwa DRC

Wiki iliyopita, Kundi la waasi la M23 lilishutumu jeshi la DRC kwa kushambulia ngome zake na kudai kwamba wanajeshi wa Burundi walikuwa wanahusika moja kwa moja katika mashambulizi hayo, serikali ya Burundi ilitoa taarifa na kufutilia mbali madai hayo.

DRC imeendelea na kusajili wanajeshi kukabiliana na kundi la M23. Viongozi hao wa jeshi wameyaagiza makundi yote yenye silaha mashariki mwa DRC kuweka chini silaha na kuacha vita. Maagizo kama hayo yamekuwa yakipuuzwa na makundi ya waasi.

Mapigano makali yamekuwa yakiendelea kati ya kundi la M23 na kikundi kinachounga mkono jeshi la serikali, cha Wazalendo katika sehemu za Kitchanga na Masisi, Kivu Kaskazini.

Rwanda ina wasiwasi mkubwa na hali ya Usalama Mmashariki mwa DRC

Mkuu wa jeshi la Rwanda Lt Gen MK Mubarakh amekiambia kikao cha Addis Ababa kwamba hali ya usalama nchini DRC inazua wasiwasi mkubwa katika eneo la Maziwa Makuu na ni swala linaloihusu sana Rwanda kwa sababu ya wimbi la wakimbizi na migogoro inayoweza kutokea.

Mubarakh ameishutumu DRC akidai kwamba inaendelea kutoa silaha kwa waasi wa FDLR na makundi yenye uhusiano na kundi hilo kwa ajili ya kusababisha usumbufu wa usalama ndani ya Rwanda.

Amesema kwamba hali ya mashariki mwa DRC ni tishio la usalama kwa Rwanda. Alisema hayo baada ya mkuu wa jeshi la DRC kushutumu Rwanda kwa matatizo ya usalama yanayoikumba DRC.

Forum

XS
SM
MD
LG