Wakati huohuo Makamu wa Rais Mike Pence amesema huenda kikosi kazi hicho kikavunjwa mnamo siku chache zijazo.
Katika ziara alioifanya Jumanne kiwanda cha kutengeneza barakoa, Arizona, Trump amesema kwamba wanarejesha nchi katika hali ya kawaida.
Rais Donald Trump, amesema :"Nawashukuru wananchi kwa kuchukuwa tadhari. Maambukizi yamepungua na kunusuru maisha ya Wamarekani wengi. Nchi yetu sasa ipo katika awamu nyingine ya kukabiliana na virusi hivi. Ipo salama kabisa na tunaanza kufungua shughuli za kawaida. Nani aliwahi kufikiria kwamba tungekuwa tunazungumzia kufungua tena shughuli za kawaida?"
Trump amewaambia waandishi wa habari kwamba Makamu wake Mike Pence na wenzake kwenye tume hiyo wamefanya kazi nzuri kabisa lakini kwa sasa, wanaangazia mtindo mwingine tofauti, ambao ni usalama wa watu na kufungua shughuli za kawaida, na huenda kuna tume nyingine itakayoundwa kusimamia suala hilo.
Trump amewaambia wafuasi wake na wafanyakazi wa kiwanda hicho kwamba anazingatia sana umuhumu wa kuhakikisha kwamba kuna utengenezaji wa bidhaa za kutosha nchini Marekani.
Lakini kwa upande wao maafisa wa afya wameonya kwamba huenda maambukizi ya virusi vya Corona yakaongezeka tena, baada ya shughuli za kawaida kufunguliwa tena.
Kulingana na hesabu ya chuo kikuu cha Johns Hopkins, watu milioni 1.2 wameambukizwa virusi vya Corona nchini Marekani, na wengine 70,000 kuaga dunia kufikia sasa.
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC