Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 19:23

Jeshi la Israeli lashambulia Gaza na Lebanon


Polisi wa Israeli wakiwa karibu na moto uliotokana na roketi zilizopigwa kutoka Lebanon na kutua Bezet, kaskazini mwa Israel, April 6, 2023.
Polisi wa Israeli wakiwa karibu na moto uliotokana na roketi zilizopigwa kutoka Lebanon na kutua Bezet, kaskazini mwa Israel, April 6, 2023.

Israel imefanya mashambulizi ya anga huko Gaza na Lebanon mapema Ijumaa, ikilipiza kisasi cha mashambulizi ya roketi kwa  Israel, serikali ikililaumu kundi la  Kiislam la Hamas.

Milipuko mikubwa yenye mitikisiko ilisikika katika baadhi ya maeneo ya Gaza wakati ndege za kivita za Israeli zikishambulia kile jeshi ilichosema ni mahandaki na maeneo ya utengenezaji silaha ya Hamas.

Jeshi la Israeli lilisema pia limelenga maeneo yenye vifaa ya Hamas huko kusini mwa Lebanon katika mashambulizi iliyofanya Ijumaa. Kituo cha televisheni cha Lebanon kilisema kulikuwa na milipuko kadhaa mji wa kusini wa bandari wa Tyre.

Jeshi lilisema linaongeza uwepo wa vikosi vyake katika mipaka ya nchi hiyo na Lebanon na Gaza “kujiandaa kwa hali zote zinazoweza kutokea.”

Mivutano ilikuwa inatokota katika eneo hilo hivi karibuni kufuatia mapigano kati ya polisi wa Israel na Wapalestina ndani ya msikiti wa Al-Aqsa mjini Jerusalem, eneo la tatu takatifu katika dini ya Kiislam.

Vurugu zilizuka tena katika msikiti wa Al-Aqsa Ijumaa kabla ya sala ya alfajiri kati ya polisi ya Israel waliokuwa na virungu na waumini wa Kipalestina wakipiga kelele za kuiunga mkono Hamas, Shirika la habari la AP liliripoti.

Wakati huo huo, maafisa wa Israel wanasema wanawake wawili waliuawa na mwingine kujeruhiwa vibaya sana katika shambulizi la bunduki lililolenga gari yao Ijumaa katika eneo linalokaliwa kimabavu huko Ukingo wa Magharibi karibu na makazi ya walowezi ya Hamra. Polisi wanasema wanawatafuta washukiwa waliofanya mauaji hayo.

Siku ya Alhamisi, Israel ilisema darzeni za mashambulizi ya roketi zilirushwa Israel kutoka katika eneo la Lebanon.

Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu alisema Ijumaa, “Hatua iliyochukuliwa na Israeli usiku wa leo na siku zijazo, itashinikiza malipo makubwa.”

Marekani, Uingereza na Umoja wa Mataifa, wakati ikitambua haki ya Israel kujihami, imesisitiza kujizuia.

Baadhi ya taarifa katika habari hii inatokana na vyanzo vya habari vya mashirika yafuatayo: The Associated Press, Agence France-Presse na Reuters.

XS
SM
MD
LG