Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Januari 24, 2025 Local time: 03:53

Historia ya mgombea urais Martin Fayulu


(FILES) Mgombea Urais Martin Fayulu Februari 2, 2019 in Kinshasa.
(FILES) Mgombea Urais Martin Fayulu Februari 2, 2019 in Kinshasa.

Martin Fayulu  si mgeni katika siasa za Congo.  Na Pia katika kinyang’anyiro cha urais ameshaonja mikimiki ya kuwania urais katika uchaguzi uliopita ambapo alishika nafasi ya pili. 

Rais Felix Tshisekedi ndiye aliibuka kidedea na kutangazwa mshindi wa urais.

Felix Tshisekedi
Felix Tshisekedi

Fayulu alizaliwa Novemba 21 mwaka 1956 katika mji uliojulikana wakati huo Leopoldvile, Belgian Congo ambao hivi sasa ni Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Licha ya kusomea fani ya uchumi na utawala na biashara, Fayulu siasa imekuwa kama ndiyo kazi yake kuu ambapo mwaka 1991 alihudhuria Mkutano Mkuu wa Taifa (Soveeign National Conference) uliowakutanisha wajumbe kutoka majimbo na mashirika mbali mbali kufanya kampeni za kudai demokrasia ya vyama vingi.

Fayulu mwenye miaka 67 ana shahada mbili za uzamili; moja katika uchumi wa jumla (General Economics) kutoka Chuo Kikuu cha Paris na nyingine katika utawala wa biashara (Business Administration) kutoka European University of America katika mji wa San Francisco nchini Marekani, aliingia kwa kasi katika siasa mwaka 2006, ambapo katika uchaguzi mkuu wa 2006 na 2011, alichaguliwa mbunge wa Bunge la Taifa, alianzisha chama cha Commitment for Citizenship and Development.

Ikumbukwa kwamba Novemba 11, mwaka 2018, Fayulu alichaguliwa na upinzani kuwa mgombea wao wa urais katika uchaguzi mkuu uliofanyika Disemba 2018, ambapo Félix Tshisekedi alitangazwa mshindi. Fayulu alishika nafasi ya pili kulingana na tume ya uchaguzi ya Congo (CENI) akiwa amepata asilimia 34.8 lakini mwenyewe anaamini alishinda kwa zaidi ya asilimia 62 ya kura na kupinga matokeo hayo mahakamani, kulingana na shirika la habari la Reuters.

Licha ya kutofaulu kile alichotarajia, hakukata tamaa na aliendeleza harakati zake za kisiasa.

Mwanasiasa wa upinzani DRC Martin Fayulu akiwa katika kampeni huko Goma.
Mwanasiasa wa upinzani DRC Martin Fayulu akiwa katika kampeni huko Goma.

Mwanasiasa huyu pia, ana uzoefu katika biashara na uchumi. Martin Fayulu ni mtendaji wa zamani wa ExxonMobil, baada ya kufanya kazi na kampuni hiyo ya mafuta kutoka 1984 hadi 2003. Alihudumu kama mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo nchini Ethiopia ikiwa ni wadhifa wake wa mwisho

Uamuzi wa Fayulu kuwania katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika siku chache zijazo, hapo awali haukuwa na uhakika kutokana na wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa udanganyifu. Hata hivyo, alitangaza nia yake ya kugombea urais hapo Septemba 30, mwaka huu. Wafuasi wake wamekuwa wakimtaja kama “muokozi” kwa hali inayoendelea huko DRC wakiamini ataleta suluhisho kwa mapigano huko mashariki mwa DRC, kuimarisha miundo mbinu, maendeleo ya uchumi, kuboresha maisha ya wa-Congo na afya. Anasema Polatisee ni mwanachama wa chama cha Engagement for Citizenship and Development (Ecide).

Ulimwengu unaiangalia DRC hivi sasa kuelekea upigaji kura wa amani, haki, na uwazi. Raia wa Congo ndio watakaoamua Disemba 20, pale watakapotumia haki yao ya kidemokrasia kumchagua kiongozi bora kwa nchi hiyo kuongoza kwa miaka mitano ijayo.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Mkamiti Kibayasi, Washington.

Forum

XS
SM
MD
LG