Mjini Bukavu katika jimbo la Kivu Kusini, vijana ndiyo wanatumiwa kubandika na hata kubandua picha na mabango ya wagombea. Vijana hao wanarandaranda huku na kule wakiwa na vyombo vya muziki, T-shirts za wagombea, bendera, na vipaza sauti ambavyo hutumika mahsusi ili kuwahamasisha raia kumpigia kura mgombea huyu au yule siku ya upigaji kura hapo Desemba 20, 2023.
Vijana hawa ambao wameshiriki kwenye mikutano ya kisiasa ya wagombea urais, wanatoa maoni yao kuelezea ambacho wanakiona kina tija kwao:
“Tunasikia kwamba tukipiga kura kwa kweli maisha ya Wakongo yataboreshwa na tutatoka kwenye dharau iliyotuathiri sisi wakongo” “Sarafu ya dola inaweza kushuka yenyewe sababu tutalima mashamba yetu na kuzalisha chakula chetu hapa, pesa zetu hazitaenda nje ila zitatunufaisha sisi Wakongo”
Bitakuya Mushaka François ni kijana mfanyabiashara ambaye anatarajia kwamba huenda uchaguzi huu utachangia kuboresha biashara yake: “Biashara yangu ni unga wa mahindi, unga wa ngano, mchele, mafuta na kadhalika. Tunakutana na changamoto nyingi kwasababu ya kupanda kwa sarafu ya dola, bei ya bidhaa imepanda pia, ndio maana tunajiandaa kushiriki katika uchaguzi ili tukitarajia hali hii itabadilika”
Hata hivyo, bado kuna vijana wengine ambao wanasita hadi sasa, wala hawajaamini kwamba uchaguzi unaopangwa DRC utaleta mabadiliko yoyote: “Nini kipya? Wamefanya nini na watafanya nini? Si ni yaleyale wamezoea kufanya. Wagombea wanatwambia tuwatume ila tukiwatuma wanapofika bungeni wananyamaza kimya, kila mtu anaujaza mfuko wake. Ile siku ya uchaguzi nitabaki nimelala kitandani” “Hata mimi naweza sema sijui kwa sababu kila mara wanasema yaleyale hakuna mabadiliko. Naona mwaka huu vijana wamejitokeza kwa wingi kugombea kuliko mwaka 2018 ila sitarajii mabadiliko. Ombi langu ni wabadilike wenyewe kama wanavyoahidi kila siku”
Na hata pia kuna wengine wanaosita kushiriki uchaguzi wakisema wanasikitishwa na chaguzi zilizopita.
Marie Nzigire ni Mkazi wa mtaa wa Bagira: “Nifiche nini? Mimi sitachagua. Tangu nimechagua nimepata nini? Ufukara, mateso, ... mambo yanaendelea kuharibika zaidi. Zamani ndio tulitarajia kupata mabadiliko ila muda huu ni zero, zero!”
Akiwa pia mgombea ubunge wa Jimbo la Kivu kusini mjini Bukavu, Dieudonné Muhigirwa ni kijana mjasiriamali. Mjasiriamali anayefanya ubunifu wa kufuga kuku. Anawataka vijana wenzake kutokata tamaa.
“Natoa mafunzo kwa vijana kuhusu kazi za mikono napia ufugaji wa kuku. Naweza zalisha vifaranga 23,000 kwa mwezi ambavyo ninagawa kwa vijana na wanawake ili wajikwamue kimaisha. Na tayari nimetoa mafunzo kwa vijana 5,000. Na ni hao vijana walionisukuma niende niwawakilishe bungeni niwe mtetezi wa wafugaji, na ninaamini tukiungana tutaweza kabisa”
Baadhi ya vijana wamejitokeza kugombea kwenye ngazi zote za uchaguzi, na wengi kati yao wanatarajia kuchaguliwa ili kuleta sura na sera mpya nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Imetayarishwa na mwandishi wetu Mitima Delachance, Bukavu, DRC
Forum