Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Septemba 25, 2024 Local time: 13:27

Guterres alaani vikali 'shambulizi kubwa' lililofanywa na kundi la RSF nchini Sudan


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema amesikitishwa sana na ripoti za shambulio kubwa dhidi ya jiji la Sudan la al-Fashir na wanamgambo wa RSF na kumtaka kiongozi wake kusitisha shambulio hilo mara moja.  

Guterres ameonya kuwa shambulizi hilo linatishia kuenea zaidi kwa mzozo katika eneo lote la magharibi mwa Darfur, kwa mujibu msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric.

"Anatoa wito kwa Luteni Jenerali Mohamed Hamdan 'Hemedti' Dagalo kuchukua hatua kwa uwajibikaji na kuamuru mara moja kusitishwa kwa shambulio la RSF," alisema Dujarric katika taarifa yake.

"Ni jambo linalotia wasiwasi kwamba pande zinazozozana zimepuuza mara kwa mara wito wa kusitisha uhasama," aliongeza.

Vita vilizuka nchini Sudan kati ya jeshi la Sudan na RSF mwezi Aprili mwaka jana, na kusababisha mzozo mkubwa zaidi wa wakimbizi duniani. Maafisa wa Umoja wa Mataifa wameonya kuwa machafuko yanayozidi kuongezeka karibu na al-Fashir yanatishia kuzua mizozo zaidi kati ya jamii.

Mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani Jake Sullivan alisema Jumamosi kwamba mzozo huo utakuwa kwenye ajenda wakati Rais Joe Biden atakapokutana na Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan siku ya Jumatatu.

Sudan na Umoja wa Falme za Kiarabu zimekabiliana katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutokana na shutuma za serikali ya Sudan inayoungwa mkono na jeshi kwamba UAE inalipatia silaha na kuliunga mkono kundi la RSF.

Forum

XS
SM
MD
LG