Tarafa ya Mugina ndio ilioathirika zaidi kutokana na mvua hizo. Mkazi wa tarafa hiyo ambaye ameongea na Sauti ya Amerika amesema familia nyingi zilipoteza watu wao, na kuongeza kuwa maporomoko hayo yaliharibu nyumba na kuteketeza mazao ya chakula.
Awali msemaji wa polisi, Pierre Nkurikiye amethibitisha kwamba watu 38 wamefariki, lakini baadae Wizara ya Usalama wa Taifa imeandika kwenye ukurusa wake wa Twitter, kwamba maporomoko hayo yamesababisha vifo 26, majeruhi 7 na wengine kumi hawajulikani mahali walipo.
Taarifa kutoka mkoani Cibitoke zinasema, raia wa eneo hilo kwa ushirikiano na polisi na shirika la mslaba mwekundu, leo asubuhi walikuwa bado wanatafuta walionusurika katika janga hilo.
Hii ni idadi kubwa ya vifo kutokea tangu miezi miwili iliyopita kufuatia mvua kubwa katika taifa hilo la Afrika ya Kati.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Patrick Nduwimana, Washington, DC