Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Desemba 26, 2024 Local time: 06:11

Sudan : Bashir atangaza hali ya dharura, aitisha mjadala wa kitaifa


Rais Omar al-Bashir
Rais Omar al-Bashir

Rais Omar al-Bashir wa Sudan Ijumaa ametangaza hali ya dharura ya taifa kwa kipindi cha mwaka moja na kuwataka waasi, wanaharakati na vyama vya upinzani kukutana na kufanya mjadala wa kitaifa.

Rais pia amezivunja serikali za mitaa na taifa na ataunda serikali mpya baada ya mjadala wa taifa kufanyika wakati maandamano yakiendelea nchini humo.

"Natoa wito kwa bunge kuchelewesha mchakato wa kurekebisha katiba kwa ajili ya kufungua milango ya kuimarisha hali ya kisiasa kupitia mijadala yenye kujenga taifa na kuchukuwa hatua za kweli za kizalendo," amesema Bashir katika hotuba yake Ijumaa jioni.

Uamuzi huo umekuja baada ya miezi miwili iliyogubikwa na maandamano yaliyosababishwa na hali mbaya ya uchumi na kuongezeka kwa bei za bidhaa, iliyopelekea kuwepo shinikizo la rais wa nchi hiyo, mwenye umri wa miaka 75, ajiuzulu.

Waandamanaji wa Sudan wakipinga serikali mjini Khartoum, Feb. 14, 2019.

Omer Ismail, mshauri wa ngazi ya juu katika mradi wa Washington-based Enough Project, amesema kuwa Bashir ametangaza hali ya dharura ya Taifa ili aweze kutangaza sheria ya kijeshi, inayompa rais amri ya kufanya maamuzi binafsi.

"Hakuna bunge, hakuna baraza la mawaziri. Yeye anaamri zote mikononi mwake. Anaweza kuamrisha jeshi kuwepo barabarani, vifaru na kikosi chochote cha jeshi," amesema Ismail.

"Vyombo vya usalama vinauhuru kuwakamata watu, kuwaweka kizuizini, kuingia majumbani mwao, kumsimamisha na kumpekuwa mtu yeyote wakati wowote."

Nchini Sudan kumekuwa na maandamano yaliyodumu tangu Disemba 19, wakati serikali ilipopandisha bei ya mkate.

Tangu wakati huo, maandamano yameongezeka na kuwepo na vurugu kati ya polisi wa kukabiliana na ghasia na waandamanaji.

Maandamano sasa yamegeuka na kuwa ya kutaka rais Omar Al-Bashir kuondoka madarakani.

Serikali ya Sudan ilisema hivi karibuni watu 31 walikufa kufuatia maandamano hayo, lakini wachunguzi wa kimataifa wa haki za kibinadamu wanasema watu 51 wameuawa.

Sudan inapanga kuandaa uchaguzi mkuu mwaka ujao 2020, na rais wa sasa Omar Al-Bashir ambaye ametawala nchi hiyo tangu mwaka 1993 baada ya mapinduzi ya kijeshi, alikuwa hapo awali ametangaza kuwania mhula wa tatu.

XS
SM
MD
LG