Waandamanaji hao wanashinikiza kuondolewa kwa wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa MONUSCO.
Maandamano hayo yamekuwa yakifanyika katika jimbo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo la Kivu Kaskazini.
Ripoti ya Msalaba Mwekundu inaeleza kwamba hospitali katika mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, Goma na mji wa Beni zina wagonjwa wengi kupindukia uwezo wao tangu April 15, kutokana na watu waliojeruhiwa, ikiwa ni pamoja na majeraha yanayotokana na risasi.
Hasira za wananchi wa jimbo hilo zimeongezeka kutokana na kuendelea kwa mauaji yanayofanywa na makundi yenye silaha na kuwasababisha wanaharakati kuitisha maandamano pamoja na mgomo katika miji mbali mbali ya jimbio hilo tangu Aprili 5 ambapo watu 10 wameshafariki.
Kulingana na takwimu za Kanisa Katholiki nchini humo watu 6,000 wameuliwa katika jimbo hilo tangu mauwaji kuanza mwaka 2013.