Afisa wa ngazi ya juu wa WHO amesema kwamba wamepokea barua kutoka kwa madaktari katika mkoa wa kaskazini wa Tigray, wakisema kwamba wameishiwa na vifaa muhimu vya matibabu ikiwemo kwa ajli ya matibabu ya kisukari.
Mkuu wa shirika la afya duniani Tedros Ghebreyesus amesema kwamba imekuwa vigumu kuwafikia watu milioni saba wanaoishi Tigray, kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja sasa.
Amesema kwamba hali hiyo imesababisha kile amekiita ni jehanamu katika eneo hilo na kwamba ni dharau kubwa kwa hali ya kibinadamu.
Ghebreyesus amesema kwamba hakuna mahali popote duniani wanashuhudia kama hali ya huko Tigray.
Dkt Ghebreyesus anaeleza : "Mkoa huu wa Tigray umezingirwa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa. Hebu fikiria kwamba watu milioni saba wamezuiliwa kabisa na hawawezi kufikiwa kwa zaidi yam waka mmoja na hakuna chakula, dawa, matibabu, umeme, mawasiliano ya simu wala vyombo vya habari. Hakuna mtu anayeweza kuripoti yanayoendelea huko.
Hakuna mawasiliano ya simu huko na kuzifikia familia ni vigumu sana. hakuan huduma kwa watu kupata pesa, hakuna huduma za benki. Hebu fikria athari za haya yote kwa afya ya binadamu. Ukosefu wa dawa una athari za moja kwa moja kwa vifo. Ukosefu wa chakula unaua. Zaidi ya hayo, mashambulizi ya mabomu yanayofanywa na ndege zisizokuwa na rubani yanaendelea kuua watu."
Mkuu huyo wa WHO anafafanua zaidi: "Kwa upande wetu kama WHO, tumekuwa tukijaribu kuwafikia watu katika eneo hilo ili kufikisha dawa katika huko Tigray na sehemu nyingine kama Afar na Amhara. Tuliruhusiwa kupeleka dawa katika maeneo ya Afar na Amhara lakini hatukuruhusiwa kuingia Tigray. Tumewasiliana na ofisi ya Waziri mkuu na pia wizara ya mambo ya nje.
Tumewasiliana na ofisi zote husika lakini hatujapewa ruhusa. Kwa hivyo, hatua za maksudi zimechukuliwa ili kuwa vigumu kwa eneo hilo kufikiwa kwa zaidi ya mwaka mmoja na kuathiri maisha ya zaidi ya watu milioni saba. Hakuna msaada wa dawa kutoka WHO, umeingia sehemu hiyo tangu mwezi July. Hakuna chochote."