Waziri Mkuu wa Sudan ajiuzulu kutokana na mgogoro wa kisiasa

Waandamanaji wakusanyika kupinga mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba 25, katika mji mkuu Khartoum, Januari 2, 2022. Photo by AFP)

Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla Hamdock Jumapili ametangaza kujiuzulu huku kukiwa na mgogoro wa kisiasa kufuatia mapinduzi ya kijeshi ambayo yanaonekana kuvuruga kipindi tete cha mpito kuelekea kidemokrasia nchini humo.

Katika hotuba yake kwa njia ya televisheni Jumapili jioni, Hamdock ambaye alitia saini mkataba wa kisiasa na jeshi mwezi Novemba amesema kwamba kuna haja ya kufanyika kwa mashauriano ili kufikia makubaliano mapya.

Hamdok ambaye ni mchumi na aliwahi kuwa afisa kwenye Umoja wa Mataifa, alishika wadhifa wa waziri mkuu katika mkataba wa kushirikiana madaraka kati ya jeshi na raia baada ya kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa muda mrefu Omar al Bashir.

FILE - Rais wa Sudan aliyepinduliwa Omar al-Bashir

Abdalla Hamdock, Waziri mkuu wa Sudan ameeleza: "Kulingana na yote niliyoyasema, nimeamua kutangaza kujiuzulu kama waziri mkuu ili kutoa nafasi kwa mwanaume au mwanamke kuhudumia taifa letu tukufu kuendeleza na kusaidia katika kipindi kilichobaki cha mpito kuelekea kuirejesha nchi katika utawala wa kiraia wa kidemokrasia.

Hamdock afisa wa zamani wa Umoja wa Mataifa, alionekana kuwa kiongozi wa ngazi ya juu wa kiraia kwenye serikali ya mpito ya Sudan, alirejeshwa madarakani mwezi Novemba huku kukiwa na shinikizo la kimataifa katika makubaliano ambayo yalitaka kuwepo kwa baraza la mawaziri la wataalam likiwa chini ya utawala wa kijeshi chini ya usimamizi wake.

Hata hivyo makubaliano hayo yalipingwa na wanaharakati wanaounga mkono demokrasia ambao walisisitiza kwamba utawala ukabidhiwe serikali ya kiraia kuongoza kipindi cha mpito.

Kujiuzulu kwa Hamdok kumekuja baada ya majeshi ya usalama ya Sudan kutumia nguvu kupita kiasi kuwatawanya waandamanaji wanaodai demokrasia waliokuwa wakipinga mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba 25, huku ripoti zikisema kwamba watu wawili walikufa kulingana na kundi la madaktari.

Hamdock anaeleza zaidi: "Hata baada ya mapinduzi ya Oktoba 25, tulitia saini muundo wa kazi na jeshi ikiwa ni jiaribio kurejea kwenye mpito wa kidemokrasia, ili kuepuka umwagikaji damu, kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa,na kulinda mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka miwili iliyopita pamoja na kuheshimu katiba iliyotumika katika kipindi cha mpito. Mkataba huu ulikuwa ni jaribio jingine la kuziunanisha pande zote na kuzileta kwenye meza ya mashauriano na kukubaliana juu ya waraka ambao utakamilisha kipindi cha mpito.

Tangazo la Hamdock sasa limeiingiza mustakbali wa kisiasa nchini humo katika hali ya ukosefu wa uhakika, miaka mitatu baada ya maandamano ya kitaifa yaliyomuondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu Omar al Bashir.

Maelfu ya waandamanaji waliingia katika mitaa ya Khartoum na miji mingine kote nchini humo ili kulipinga jeshi kujinyakulia madaraka, na hatimaye kufikia makubaliano na kumrejesha madarakani waziri mkuu lakini wakalitenga vuguvugu la demokrasia.

Kamati kuu ya madaktari wa Sudan CCSD ambayo ni sehemu ya vuguvugu linalounga mkono demokrasia Jumapili imesema kwamba mmoja wa watu alikufa kwenye maandamano ya mwishoni mwa wiki alipigwa kwenye kichwa mjini Khartoum.

Wa pili alipigwa risasi kwenye kifua kwenye mji pacha wa Khartoum wa Omdurman wakati darzeni ya waandamanaji walijeruhiwa kulingana na kundi hilo.

Vifo vya Jumapili vimefikisha jumla ya watu 56 tangu mapinduzi ya kijeshi kulingana na kundi la madaktari.

Jenerali Abdel Fattah al-Burhan

Kiongozi wa kijeshi generali Abdel Fattah al Burhan amesema Jumamosi kwamba taifa hilo linakabiliwa na tishio huku kukiwa na hali ya ghasia baada ya mapinduzi ya kijeshi zaidi ya miezi miwili iliopita.

Abdel Fattah al Burhan, Kiongozi wa kijeshi anaeleza: Nyote mnaelewa hali tunayopitia kama taifa, pamoja na changamoto zinazotishia uthabiti wa taifa. Ni tishio tulilo nalo na ambalo hatuwezi kuliepuka ila kukabiliana nalo tukiwa na uzalendo wakati tukiweka maslahi ya taifa mbele.

Hamdok ametoa wito wa kuwepo na majadiliano ili kukabiliana juu makkubaliano ya kitaifa pamoja na mchakato kukamilisha mpito kamili.

Waziri Mkuu wa Sudan alitoa wito: Nachukua nafasi hii kushukuru watu wote ulimwenguni wanaounga mkono uhuru amani na haki, pamoja na wale wanaoamini haya mapinduzi ya watu hawa wa maana. Msimamo wenu katika kuunga mkono juhudi za watu wa Sudan pamoja na haki yao ya uhuru hakika hautasahaulika, wakati tukiamini kwamba mtaendelea kutusaidia.

Mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba yalihujumu juhudi za mpito wa kidemokrasia kufuatia maandamano yaliyopelekea kuondolewa kwa kiongozi wa muda mrefu Omar al Bashir pamoja na serikali yake Aprili 2019.