Waziri Mkuu wa Congo atishia serikali kuvunjika kwa kukamatwa waziri

PrésidentFélix Tshisekedi na likita lya mbulamatari, na téléconférence, na cité ya Union africaine, Kinshasa, 26 juin 2020. (Facebook/Présidence RDC)

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) amepinga kitendo cha kukamatwa kwa waziri wa sheria, akisema serikali ya mseto inaweza kuvunjika juu ya suala hilo na kumtaka rais kuwahakikishia mawaziri utetezi wa kisheria.

Waziri wa Sheria Celestin Tunda alikamatwa na polisi Jumamosi jioni na kuachiwa baada ya saa kadhaa za kuhojiwa na waendesha mashtaka katika mahakama, na kusababisha mgogoro wa kisiasa katika serikali ya mseto iliyoko madarakani, Shirika la Habari la Reuters limeripoti.

“Hili suala nyeti na ambalo halijawahi kutokea linaweza kudhoofisha utulivu na utendaji wa mshikamano wa taasisi mbalimbali, na kusababisha serikali kuvunjika,” Waziri Mkuu Sylvestre Ilunga amesema katika tamko rasmi.

Tunda amekwaruzana na Rais Felix Tshisekedi juu ya mabadiliko ya mahakama yaliyopendekezwa na chama cha Tunda ambayo yataipa wizara ya sheria udhibiti zaidi juu ya uendeshaji wa kesi za jinai.

Wale wanaopinga mabadiliko hayo wanasema yatadumaza uhuru wa mahakama.

Kutokubaliana huko kumeonyesha mvutano uliopo katika serikali ya mseto baina ya Tshisekedi na washirika wa mrithi wake aliyekuwa madarakani kwa muda mrefu, Joseph Kabila.

Kabila aliachia madaraka mwaka jana lakini anaendelea kuwa na madaraka mapana kupitia wawakilishi wake walio wengi bungeni na kuwa wanashikilia wizara nyingi na ofisi ya waziri mkuu. Tunda anasauti katika chama cha PPRD cha Kabila.

“Hakuna kiongozi wa serikali ambaye anaweza kushtakiwa kwa sababu ya maoni yaliotolewa wakati wa majadiliano ya baraza la mawaziri,” Ilunga amesema akirejea mkutano wa Ijumaa ambapo Tshisekedi na Tunda walikwaruzana juu ya mabadiliko ya mahakama.

Ilunga alisema mahakimu waliohusika katika kile alichokiita “ukamatwaji wa kikatili na kiholela” wa Tunda lazima wachukuliwe hatua za kisheria.

Tshisekedi aliingia madarakani Januari 2019, na kuunda serikali ya mseto kwa kushirikiana na Kabila, lakini muungano huo umeendelea kuonyesha dalili za kutokuwepo mshikamano.

Maelfu ya waandamanaji walijumuika kupinga sheria hiyo iliyopangwa katika viwanja vya bunge Jumatano. Walitimuliwa na polisi waliotumia mabomu ya kutoa machozi na maji yenye kuruka kwa nguvu.