Watu 13 washtakiwa kwa kumtishia kumuua mkosoaji wa Uislam

Loubna, msichana wa Morocco mwenye umri wa miaka 18 aliyelengwa na unyanyasaji wa mitandao akitumia simu yake mji wa mwambao wa Casablanca Machi 9, 2020. (Photo by FADEL SENNA / AFP)-

Watu 13 wamefikishwa mahakamani, Jumatatu, mjini Paris, wakituhumiwa kwa unyanyasaji kupitia mtandao au kutoa vitisho vya kutaka kumuua msichana mwenye umri wa miaka 18 aliyechapisha matamshi ya kuukosoa Uislamu.

Hiyo ni kesi ya kwanza ya aina yake chini ya mahakama mpya iliyoundwa Ufaransa mwaka 2021 ili kuhukumu uhalifu wa mtandao ikiwa ni pamoja na unyanyasaji na ubaguzi.

Washtakiwa ambao ni watu kati ya umri wa miaka 18 hadi 35 na kutoka maeneo mbalimbali ya Ufaransa wanakabiliwa na hukumu ya miaka miwili jela na faini ya hadi Euros 30,000 wakipatikana na hatia ya unyanyasaji wa mtandaoni.

Msichana aliyelengwa na vitisho na kujitambulisha kama Mila kwenye ukurasa wake wa mtandao alisambaza video iliyoenea sana mwaka 2020 kwenye ukurasa wa Instagram na TikTok zilizokuwa zinaukosoa Uislamu na Quran.

Kufuatia usambazaji huo alipokea vitisho vya kuuliwa na unyanyasaji wa kila aina kwenye mtandao na hivyo kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi na kuhamishwa shule.

Chanzo cha Habari : AP