Wataliban wauteka mji wa Ghazni wakisonga mbele kuelekea Kabul

Wapiganaji wa Taliban wakifanya doria katika mji wa Ghazni, Kusini magharibi ya Kabul, Afghanistan, Alhamisi, Agosti 12, 2021. (AP Photo/Gulabuddin Amiri)

Wapiganaji wa Taliban wameuteka mji mkuu wa tisa, Ghazni, Alhamisi nchini Afghanistan.

Ghazini ni miongoni mwa miji mikuu ya majimbo ya nchi hiyo ambayo wameikamata wiki hii.

Wakati huohuo upelelezi wa Marekani unasema mji mkuu wa Afghanistan, Kabul, ulio mwendo wa saa chache kutoka Wataliban walipo huenda ukaangukia katika mikononi mwao ndani ya siku 90.

Kasi ya kusonga mbele kwa Taliban imesababisha kusambaa kwa malalamiko juu ya uamuzi wa rais Joe Biden kuondoa vikosi vya Marekani na kuiacha serikali ya Afghanistan kupigana peke yake.

Wakati vikosi vya mwisho vya kimataifa vinavyoongozwa na Marekani vikitarajiwa kuondoka mwishoni mwa mwezi huu kundi la Taliban limechukua udhibiti wa takriban theluthi mbili y Afhghanistan wakiwa wamefanya mashambulizi pande nyingi.

Imekuwa vigumu kwa wilaya na vijijini kujitetea wenyewe, kufuati vikosi vya serikali kuondoka maeneo hayo kwa ajili ya kuihami Kabul na miji mingine na hivyo kusababisha maelfu ya familia kukimbia majimbo kwa matumini ya kutafuta usalama.