Imani za kitamaduni zinawaweka wanawake kama watu wa daraja la chini kwa wanaume na hivyo kudhoofisha juhudi za kisheria kuhakikisha wanawake wanapata haki sawa juu ya ardhi.
Ushirika mpya wa wanawake unalenga kupambana na imani hizi na kuwasaidia wanawake kudai haki zao. Mwanamke mmoja aliyeondoka katika ndoa yenye manyanyaso alisema, "kama wanawake wasingekuwa wanapoteza mashamba, wangeweza kuthubutu kuondoka kwa waume zao mapema." Wataalamu wanasema pia kuwa wanawake wenye sauti juu ya ardhi mara nyingi wanatumia mbinu za kilimo endelevu.
Milla Nemoudji, mwenye umri wa miaka 28 kutoka kijiji kimoja kusini mwa Chad, alipoachana na mume wake baada ya miaka mingi ya manyanyaso, alijikuta hana njia ya kujikimu kimaisha. Ingawa alikulia katika familia ya wakulima, alipata shida kujikimu katika jamii ambako upatikanaji wa ardhi humilikiwa na wanaume.
Kukiwa na msaada mdogo kwa wanawake walio katika hali kama yake, na kutalikiana ni nadra nchini Chad, alijitahidi kupata uhuru wa kiuchumi. Aliuza matunda na bidhaa nyingine. Wakati wa msimu wa mvua, alilima mashamba kama kibarua.
Hata hivyo, mwaka jana, kikundi cha wanawake kilifika kijijini kwake na akaamua kujiunga, hatimaye akapata ardhi na sauti juu ya matumizi yake. Alilima pamba, karanga, na kupata pesa za kutosha kugharamia mahitaji ya msingi.
Kijiji cha Binmar kiko pembeni mwa mji wa pili kwa ukubwa nchini Chad, Moundou, katika mkoa wenye idadi kubwa ya watu wa Logone Occidental.
Fursa ya kuwa na ardhi nchini Chad mara nyingi hudhibitiwa na machifu wa vijiji ambao huhitaji malipo ya kila mwaka. Wanawake mara nyingi hutengwa katika umiliki wa ardhi na urithi, na hivyo kuwafanya wawe tegemezi kwa wanaume katika jamii.
Mapambano ya haki za ardhi yanakabiliwa na changamoto nyingi na mfumo maradufu wa kisheria nchini Chad ambapo sheria za kimila mara nyingi hutangulizwa juu ya sheria za serikali, hasa vijijini. Ingawa mageuzi ya kisheria ya hivi karibuni yameifanya sheria kutambua haki ya raia yeyote kumiliki ardhi, utekelezaji wa sheria hizo bado haujashika kasi.
Kwa wanawake kama Nemoudji wanaodai haki zao, majibu yanaweza kuwa ya uhasama.
“Hakuna mtu anayekuja kukusaidia, ingawa kila mtu anajua kwamba unateseka,” Nemoudji aliiambia Associated Press, akikosoa mfumo wa jadi wa haki za ardhi na kuwataka viongozi wa maeneo ya kiasili kuliangalia kwa umakini suala la manyanyaso ya majumbani. "Kama wanawake wasingekuwa wanapoteza mashamba, wangeweza kuthubutu kuondoka kwa waume zao mapema."
Mikakati kama ya N-Bio Solutions, kikundi ambacho Nemoudji alijiunga nacho, una changamoto kwa taratibu hizo. Ilianzishwa na Adèle Noudjilembaye mwaka 2018, mtaalamu wa kilimo na mwanaharakati kutoka kijiji jirani, kikundi hiki ni mpango nadra nchini Chad unaofanya mashauriano kwa niaba ya wanawake na machifu wa jadi, ambao kisha hutafuta wakazi walio na ardhi na kuikodisha.
Hadi sasa, Noudjilembaye anaendesha vikundi vitano kama hivyo vyeny wastani wa wanachama 25. Ingawa mikakati hii inapata umaarufu polepole, inakabiliwa na ukomo wa rasilimali za kifedha na hofu ya wanawake wengine kuhatarisha kidogo walicho nacho.
Noudjilembaye aliiambia AP kwamba “licha ya vurugu na kutelekezwa, wanawake wengi wanabaki katika hali hiyo kwa sababu ya utegemezi wa kifedha, hofu ya kuhumiwa na jamii au ukosefu wa misaada.”
Jitihada za pamoja za makundi kama haya zina athari kubwa kwa usawa wa kinsia na kilimo endelevu nchini Chad. Wanawake wa Binmar wanatumia mbinu za kilimo endelevu ikiwa ni pamoja na mzunguko wa mazao, kilimo cha kikaboni na matumizi ya mbegu zinazostahimili ukame, ambazo husaidia kuhifadhi udongo na kuongeza uzalishaji.
Kwa ujumla, wanawake wanaomiliki ardhi na rasilimali wana uwezekano mkubwa wa kutekeleza mbinu za kilimo endelevu na kuboresha mifumo ya chakula ya ndani, kulingana na Umoja wa Mataifa.
Lakini nchini Chad, maisha ya wanawake wanaojaribu kudai haki zao ni changamoto kubwa.
Chad imeorodheshwa ya 144 kati ya nchi 146, kulingana na ripoti ya 2024 ya Global Gender Gap iliyokusanywa na World Economic Forum. Kiwango cha vifo vya akina mama wakati wa kujifungua kiko juu kwa vifo 1,063 kwa kila watoto 100,00 waliozaliwa mwaka 2020, zaidi ya mara tatu ya wastani wa kimataifa, kulingana na Umoja wa Mataifa. Ni asilimia 20 tu ya wanawake vijana wanajua kusoma na kuandika.