Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 22, 2024 Local time: 08:11

Ukeketaji wa wanawake waendelea kuwa tatizo katika jamii ya Kimaasai


Wamaasai wanaoishi mpakani mwa Tanzania na Kenya. Picha na TONY KARUMBA / AFP
Wamaasai wanaoishi mpakani mwa Tanzania na Kenya. Picha na TONY KARUMBA / AFP

Mila ya Ukeketaji wanawake maarufu kama FGM bado ni tatizo katika jamii ya wafugaji wa kimaasai nchini Tanzania.

aKwa mujibu wa takwimu za karibuni mkoa wa Manyara uliopo kaskazini mwa taifa unaongoza kwa visa vingi vya wanawake na wasichana kupitia mila ya ukeketaji. Utaratibu huu unafanyaika kwa siri na hata wasichana wadogo wanafanyiwa hivyo, lakini baadhi ya wazee wanaamini mila hii ya tohara ni muhimu kwa maadili ya jamii kwani ndiyo mafunzo muhimu ya makuzi yanayostahili.

Kulingana na tamaduni za kimaasai mwaka wowote unaogawanyika kwa mbili ni mwaka rasmi wa kufanyika kwa utaratibu wa tohara, licha ya serikali kupiga marufuku ukeketaji wanawake, lakini mila hii ni kilio kikubwa kwa wasichana wa kimaasai.

Utaratibu huu wa kimila hufanyika kwa usiri mkubwa ambapo wasichana wadogo ni kundi ambalo liko hatarini zaidi

Mwanamke wa Kimaasai Theresia Peter ameiambia Sauti ya amerika “Tunapiga vita kutokomeza mila hii, kwa sababu ina maumivu makubwa kwa wasichana wadogo na mara nyingine husababisha kifo’’

Elimu ni moja kati ya silaha muhimu inayotumiwa na serikali kukabiliana na ukeketaji ambao pia ni kichocheo cha ndoa za utotoni katika jamii ya wamaasai. Baadhi yao wanaamini elimu na kutangamana na jamii nyin gine kunafanya utamaduni wao kuendelea kufifia nahata kusababisha kuporomoka kwa maadili.

“Zamani wamaasai walikuwa hawasomeshi watoto wasichana, lakini kadri miaka inavyokwenda sasa wasichana wanasoma wanajichanganya na jamii nyingine na wanapojichanganya ndipo wanapojifunza,” alisema Peter.

Rais wa zamani wa Marekani alipowatembelea wanafunzi wa elimu ya watu wazima katika shule ya wasichana ya Wamaasai huko Tanzania
Rais wa zamani wa Marekani alipowatembelea wanafunzi wa elimu ya watu wazima katika shule ya wasichana ya Wamaasai huko Tanzania

“kwa wale wanaotumia simu wanaingia katika mitandao ya kijamii ambayo pengine inawaharibu, kwa hiyo elimu ni nzuri lakini imeharibu maadili ya kimaasai,” aliongeza.

Kiwango cha ukeketaji nchini Tanzania kinaelezewa kimeshuka kwa zaidi ya asilimia 90 hii ni kutokana na elimu na sheria kali ambazo zimewekwa katika taifa hili la Afrika ya Mashariki.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa wasichana wenye umri wa miaka kati ya 15 na 45 wamepitia utaratibu wa ukeketaji na asilimia 35 walikeketwa wakiwa na umri wachini ya mwaka mmoja barani Afrika.

Viongozi wa kimila wanasema ukeketaji si mila potofu ni hatua muhimu kwa makuzi ya wasichana kutokana na mafunzo yanayotolewa.

Akizungumza kuhusiana na mila hiyo Lekoko Piniel Ole Lepilal alisema “Ukeketaji sio mila potofu ilikuwepo na kulikuwa na sababu ya kufanya ukeketaji lakini hatuendelezi kwa sababu ya elimu ndani ya jamii kuhusiana na baadhi ya mambo.

Wanawake wa Kimaasai wakiimba wakati wa kutawazwa kwa kiongozi wa rika wa kundi la Morani
Wanawake wa Kimaasai wakiimba wakati wa kutawazwa kwa kiongozi wa rika wa kundi la Morani

Amesema “Sisi hatusemi ukeketaji, mwanamme anaingia jandoni mwanamke anawekwa unyago. Wanasema unapomtahiri mwanamme na mwanamke anatoka kwenye hatua ya utoto na kuingia utu uzima, upotofu unakuja pale ambapo watu hawaelewi mafunzo, ndio maana sasa kila mtu anamlaumu kijana sababu hakuna elimu inatolewa kwa vijana ili waendane na maisha ya ndoa na maisha ya utu uzima.”

Utamaduni wa kimaasai umekuwa kivutio kikubwa kwa miaka mingi lakini miaka ya mbeleni kuna hofu ya kufifia au kutoweka kabisa.

Kati ya wanawake zaidi ya milioni 200 waliokeketwa duniani kote asilimia 50 ni kutoka bara la Afrika huku kwa nchi za Afrika Mashariki zinaelezewa zina viwango vya juu vya ukeketaji. Kwa mfano Kenya ina matukio mengi ya ukeketaji kwa siku za hivi karibuni ikiwa na asilimia 27 huku Uganda ikiwa mfano wa kuigwa ikiwa na asilimia moja tu.

Wanaharakati wa haki za wanawake nchini Tanzania wamekuwa mstari wa mbele kuzungumzia upigaji marufuku wa mila potofu kama vile ukeketaji wanawake na wasichana hali ambayo huwaacha baadhi ya wale wanaopitia utaratibu huu kuwa athari za kiafya na kimwili na wengine wanadaiwa kupoteza maisha.

Forum

XS
SM
MD
LG