Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 15, 2025 Local time: 13:52

Ususi unawawezesha wanawake Kigali kujikimu na kutunza familia


Mmoja wa wanawake wanaofanya kazi ya ususi katika jiji la Kigali
Mmoja wa wanawake wanaofanya kazi ya ususi katika jiji la Kigali

Wanawake wengi wanaojihusisha na ususi katika jiji la Kigali nchini Rwanda wanaisifia kazi yao kwa kuwapatia kipato cha kuwawezesha kujikimu na kutunza familia zao.

Wakizungumza na sauti ya Amerika wanawake hao wasusi ambao hufanyia kazi zao kwenye saluni, na baadhi yao huwafuata wateja majumbani mwao, wanawahamasisha wanawake wenzao kujishughulisha na kazi zozote ambazo zitawapatia kipato badala ya kukaa nyumbani bila ya kazi.

Aidha wamesema, kazi ya ususi inawawezesha wanawake wengi kutunza familia, na kukabiliana na ukosefu wa ajira nchini Rwanda.

Sauti ya Amerika imetembelea moja ya saluni zilizopo katikati ya mji wa Kigali na kukutana na wateja wengi amba0 wamefika kwa ajili ya kufanya usafi wa nywele pamoja na kusuka.

Wasusi wameelezea faida wanazozipata kutokana na kazi hiyo, Francine Uwitonze anasema huu ni mwaka wa 22, anafanya kazi ya ususi, akisisitiza kuwa imempa mafanikio mengi kama vile kulipia na kuwasomesha watoto wake.

“Nina miaka 22 nafanya hii kazi ya kusuka, ni kazi nzuri, kwa mfano mimi nina watoto watatu wawili wapo shule ya sekondari na wa watu ni mdogo, wote wana maisha mazuri kutokana na kazi yangu ya kusuka” alisema Uwitonze.

mteja akisuka nywele saluni huko Kigali
mteja akisuka nywele saluni huko Kigali

Faida ya kazi ya ususi wa nywele pia znatajwa na wanawake wengine wanaojishughulisha na kazi hizo ni kuwahamasisha wanawake wenzao kuweza kujifunza kazi hiyo.

Naye Assouma Mbabazi amesema, Hatuwezi kulala njaa, hatuwezi kukosa kodi ya nyumba, ukikosa kazi leo unapata kesho, hatuna tatizo, tunasaidia familia zetu, wanawake wasiidharau hii kazi ya kusuka,mwanamke msusi hawezi kukosa pesa za kuwasaidia watoto.”

“Na wewe ndio unajipangia kazi, unaweza kuja kazini ukiwa umemaliza kuweka sawa mambo ya nyumbani, nawaambia wanawake wenzangu waje wajifunze kazi ya mikono ni kazi ambayo huwezi ukakosa pesa ya kusaidia familia,” amesema Mbabazi. “Mimi kama mwanamke naipenda kazi ya ususi, nimefanya hii kazi nikiwa bado mwanafunzi, imenisaidia kulipa ada ya shule na nimemaliza shule naendelea na kazi yangu ya ususi,” aliongeza.

Licha ya kazi ya ususi kusifiwa sana na wanawake hao, kwa upande mwingine pia wanazitaja changamoto wanazokumbana nazo pamoja na fikra potofu za baadhi ya wateja wanaodharau kazi hiyo.

Akizungumzia changamoto hizo Uwitonze amesema “Kazi ya kusuka ina changamoto zake, kudharauliwa na wateja ,hasa wale tunaowakuta majumbani ,wanadharau kazi yetu ,na tunaomba wateja wetu waheshimu hii kazi yetu, tunapokwenda kwao ni kama wao wanapokwenda ofisini kwao, mtu anapokukuta nyumbani mheshimu na uheshimu kazi yake”.

Ripoti zinazotolewa zinaonyesha changamoto ya ukosefu wa ajira ni swala gumu duniani, na wanawake wakiongoza kwa idadi kubwa ya ukosefu wa ajira, Rwanda imewekeza kwenye mafunzo ya ufundi stadi, ikiwemo kufundisha kazi za saluni ili kupambana na changamoto hiyo.

Imetayarishwa na Edith Nibakwe, Sauti ya Amerika, Kigali Rwanda

Forum

XS
SM
MD
LG