Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Novemba 22, 2024 Local time: 19:33

Wanawake wanatakiwa kuwa wabunifu kutatua changamoto za kibiashara Tanzania


wanawake wachimba migodi wa tanzania wakitembea pamoja wakati wa magharibi Mei 262022. Picha na LUIS TATO / AFP
wanawake wachimba migodi wa tanzania wakitembea pamoja wakati wa magharibi Mei 262022. Picha na LUIS TATO / AFP

Wanawake Tanzania watakiwa kuwa wabunifu na kujenga tabia ya kukimbilia fursa mbalimbali zinapojitokeza wakati serikali ikiahidi kushirikiana na sekta binafsi katika kutatua changamoto za kibiashara wanazokumbana nazo wanawake nchini humo.

Wakizungumza na Sauti ya Amerika pembeni ya mkutano wa Wanawake wafanyabiashara ndani ya eneo huru la biashara Afrika (AfCFTA) uliofanyika jiji Dar es salaam, wamesema bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa katika kuandaa bidhaa zao ili kufikia masoko mbalimbali barani humo.

Miongoni mwa changamoto hizo wamezitaja kuwa ni upatikanaji wa malighafi za kutengenezea bidhaa kwa muda muafaka, ukosefu wa vifungashio bora pamoja na wanawake wengi kutokuwa na mitaji inayojitosheleza.

Fatuma Riyami ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Nature Ripe Killimanjaro Ltd ameiambia Sauti ya Amerika kuwa wanawake wanatakiwa kuwa wabunifu katika kukabiana na changamoto za kibiashara, na kueleza jinzi yeye binafsi alivyokabiliana na baadhi ya changamoto za upatikanaji wa malighafi kwenye shamba lake.

“Changamoto za kupata mazao ya wakulima kwa muda sahihi kwasababu watu wengi wanatumia mvua kuotesha mazao kwahiyo siku nyingine unaweza usipate kabisa malighafi hizo” alisema Riyami.

Aliongeza “ndio maana mimi kwenye shamba langu nimeanza kupanda vile vitu ambavyo natumia kuzalisha bidhaa zangu ninapanda pilipili, maembe, nina karanga kwahiyo inabidi niwe na akiba kutoka kwenye shamba langu ili niweze kusindika kwa mwaka mzima.”

Wanawake wakinunua samaki katika soko la Samaki lililopo Kivukoni Dar Es Salaam. Picha na AFP
Wanawake wakinunua samaki katika soko la Samaki lililopo Kivukoni Dar Es Salaam. Picha na AFP

Kulingana na takwimu zilizotolewa na Katibu Mkuu wa (AfCFTA) Mwamkele Mene. Aslimia 90 ya biashara zote barani Afrika ni biashara ndogondogo na za kati. Miongoni mwao ni asilimia 60 zinazomilikiwa na wanawake na kuchangia asilimia 80 ya uzalishaji wa ajira na kuchangia asilimia 40 ya pato la taifa la Afrika.

Naye mkurugenzi wa kampuni ya AJAT limited iliyopo nchini Tanzania Happiness Abisa, amewataka wanawake kujenga tabia ya kuzikimbilia fursa pale zinapojitokeza na kuacha kuhofia changamoto kwakuwa changamoto ndio zinatoa nafasi ya kujifunza zaidi.

“Fursa zinapokuja usiiache ukasikia kama hadithi ichukue ifanyie kazi changamoto utakazokutana nazo ni ndogo ambazo utajifunza na utasonga mbele kwahiyo mimi niwashauri wanawake ambao wanataka kuingia kwenye hili soko cha kwanza wawe na bidhaa zenye ubora zilizofungashwa vizuri na ziwe na bei nzuri pia.” Alisema Abisai.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Viwanda na Biashara Ashatu Kijazi imeahidi kufanya kazi na sekta binafsi ili kutatua changamoto za wafanyabiashara wanawake wanazopambana nazo ili kuwanyanyua kiuchumi.

Alisema “kama wizara kwa niaba ya serikali tunakuhakikishia tutaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na sekta binafsi na kuwawezesha kushughulikia changamoto wanazokumbana nazo ili tuendelee kumnyanyua mwanamke ndani ya taifa letu la Tanzania.”

Ikiwa siku ya pili wa mkutano wa wafanyabiashara wanawake barani Afrika, mkutano ambao unaendelea kuibua changamoto za wanawake hao ambapo mjadala wa ufumbuzi unatarajiwa utafanyika siku ya Ijumaa ambapo mkutanohuo unamalizika.

Imetayarishwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Dar es Salaam

Forum

XS
SM
MD
LG