Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 03:43

Wavuvi Tanzania wataka ruzuku na kushirikishwa katika mabadiliko ya sheria za uvuvi.


Wavuvi huko Zanzibar. PICHA na AFP / GABRIEL BOUYS.
Wavuvi huko Zanzibar. PICHA na AFP / GABRIEL BOUYS.

Wavuvi nchini Tanzania wameitaka Serikali kuweka ruzuku katika sekta ya uvuvi ili kupunguza gharama za uvuvi na kutokomeza uvuvi haramu ili kusaidia kulinda mazalia ya samaki.

Wavuvi nchini Tanzania wameitaka Serikali kuweka ruzuku katika sekta ya uvuvi ili kupunguza gharama za uvuvi na kutokomeza uvuvi haramu ili kusaidia kulinda mazalia ya samaki.

Katika maadhimisho ya siku ya uvuvi duniani, wavuvi hao, wameomba washirikishwe katika mabadiliko ya sheria na kanuni za uvuvi, wamesema ruzuku katika sekta ya uvuvi inaweza kuwa njia muhimu ya kuwasaidia wavuvi kupunguza gharama zao na kuboresha maisha.

Wamesema ruzuku ya serikali ya inaweza kuhamasisha matumizi bora ya rasilimali za uvuvi na kuchangia katika kudhibiti uvuvi haramu.

Msemaji wa Chama Cha Wavuvi Tanzania (TAFU) Sijaona James kutoka Mwanza ameiambia Sauti ya Amerika, serikali inapaswa kulitazama suala la ruzuku ikiwa inataka kuwatoa wavuvi katika lindi la umaskini na kuhakikisha sekta ya uvuvi inachangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la taifa.

Wavuvi katika Soko la Samaki la Malindi lililopo Mji Mkongwe, Zanzibar Desemba 28, 2017.
Wavuvi katika Soko la Samaki la Malindi lililopo Mji Mkongwe, Zanzibar Desemba 28, 2017.

Amesema “Namna sekta ya uvuvi ilivyotelekezwa inachangia sana kudhoofisha mapato na mwisho wa siku haiwezi kuonekana kama ina mchango wowote kwa taifa, tusisitize kwamba ruzuku ni muhimu sana kwenye sekta ya uvuvi kama tunataka kuwasaidia wavuvi kuvua vizuri kwa faida na kujenga utajiri wa taifa letu na hasa kubadilisha maisha ya wavuvi ili kujitoa kwenye hali ya umaskini.”

Serikali ya Tanzania, kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), inatekeleza mpango wa kutoa jumla ya boti 160 zenye thamani ya bilioni 11.5 kwa ajili ya wavuvi nchi nzima. Hatua ambayo inalenga kuimarisha uwezo wa wavuvi na pia kutoa ajira za moja kwa moja kwa takribani wavuvi 4,296.

Suala ambalo baadhi ya wavuvi walioanza kunufaika na mradi huo wametoa mrejesho hasi na kusema kwamba mpango huo haujawa na manufaa wanayotarajia kutokana na Serikali kushindwa kuwashirikisha kikamilifu tangu awali, kama Mkuu Kizigo mvuvi kutoka Pangani aliiambia Sauti ya Amerika

“Serikali wakati inapofanya mambo yake ishuke chini kwa wenyewe ili waelezwe mambo gani wanayoyataka, hiyo ni changamoto kwa hivi vyombo ambavyo vimetoka vinachangamoto kubwa sana,”alisema Kizito

Wavuvi katika soko la samaki la Kivukoni Dar es Salaam.
Wavuvi katika soko la samaki la Kivukoni Dar es Salaam.

Hata hivyo uwepo wa mabadiliko ya sheria na kanuni za uvuvi inayokataza baadhi ya shughuli za uvuvi kufanyika mchana na kuruhusu usiku imekuwa ni miongoni mwa changamoto kwa wavuvi na kuitaka serikali kukaa na wavuvi ili kuitazama sheria hiyo.

Akilizungumzia sula hilo Sefu Isumaili kutoka Kigamboni Mnazi Mkinda alisema

“Kama zana ni haramu maana yake ni haramu mchana na usiku, haziwezi kuwa haramu mchana na usiku ni halali, na tukawaambia kwamba hii sheria inaonekana haikufanyiwa utafiti.” “Kweli walituelewa na baadhi yao wakabaini ile sheria haikufanyiwa utafiti. Lakini mpaka leo hii ile sheria haijafutwa, ikiwezekana serikali ituite tukae nao tutafute ufumbuzi wa pamoja” Isumaili aliongeza.

Madhimisho ya siku ya uvuvi nchini Tanzania yamebeba kauli mbiu inayosema "Uvuvi endelevu kwa maendeleo ya uchumi wa bluu" ikilenga kuhamasisha na kutoa mwongozo kwa wadau wote wa sekta ya uvuvi kuhusu umuhimu wa kutekeleza mbinu endelevu za uvuvi na matumizi bora ya rasilimali za bahari.

Imetayarishwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Dar es Salaam

Forum

XS
SM
MD
LG