Tuhuma hizo zimekuwa zikielezewa katika ya ripoti ya Mkaguzi Mkuu kwa muda wa miaka mitatu mfululizo.
Wakizungumza na Sauti ya Amerika, wamesema licha ya ripoti hizo kufikishwa bungeni na kufanyiwa uchambuzi na kamati za bunge, lakini hakuna hatua iliyochukuliwa kwa baadhi ya watumishi waliohusika na ubadhirifu wa fedha za umma kama ilivyotajwa na ripoti za CAG.
Dennis Konga Mhadhiri kutoka Chuo cha Diplomasia Dar es Salaam aliiambia Sauti ya Amerika kuwa ni wakati kwa wananchi kuamua mustakabali wa nchi yao kwa kuwahoji wawakilishi wao kuhusu hatua za kuchukua dhidi ya wabadhirifu ili kuhakikisha mabadiliko yanatokea ndani ya serikali pamoja na ndani ya mifumo ya utawala.
“Lakini pia ni nafasi ya wananchi kuweza kuamua mustakabali wa nchi yao wenyewe na tuhoji kwa maana ya kwamba tunataka kuona mabadiliko makubwa yanatokea ndani ya serikali na ndani ya mifumo yetu ya utawala.” Alisema Konga.
Wenyeviti wa kamati wakiwasilisha mapendekezo ya kamati zao wameitaka kamati kuu ya Bunge kufuatilia mapendekezo yaliyotolewa na wabunge ya kuitaka serikali kuwashughulikia watuhumiwa hao wa ubadhirifu wa mali ya umma.
Mwandishi wa habari mkongwe na mwanasheria, Jenerali Ulimwengu, ambaye ameonyesha wasiwasi kuhusu utendaji wa kamati hiyo kwa jinsi inavyotekeleza majukumu yake.
Amesema kamati hiyo imeathiriwa na serikali na inashindwa kutekeleza jukumu lake la kuibana serikali katika matumizi ya fedha za umma.
“Kamati hiyo haijawahi kufanya kazi yake kama ilivyokusudiwa na imekuwa ikifanya kama inavyotaka serikali. Kamati hiyo haijawahi kuwa na uwezo wa kuidhibiti serikali katika matumizi ya fedha za wananchi” Alisema Ulimwengu
“Kwahiyo sitarajii kwamba kutatokea jambo lolote jipya ambalo litaibana serikali na kupunguza ubadhirifu ambao tumeuona katika matumizi ya serikali” aliongeza.
Naye Mjumbe wa kamati kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Heche aliiambia Sauti ya Amerika kuwa Bunge lilipaswa kuchukua hatua kwa kumtaka Rais kulivunja baraza la mawaziri na kupitisha maazimio ya kuwachukulia hatua wabadhirifu wote wa mali ya umma.
“Wabunge wa chama tawala walipaswa kuchukua hatua. wana mamlaka hiyo kwa mujibu wa ibara ya 63 ya katiba ya nchi yetu wangepiga kura wangeweka maazimio ya kumtaka Rais avunje baraza la mawaziri na aliunde upya wapitishe maazimio ya kuwachukulia wabadhirifu hatua.” Alisema
Miongoni mwa maazimio yaliyofikiwa na bunge katika mjadala huo ni pamoja na kuwataka mawaziri, makatibu wakuu na viongozi wengine waliotajwa kwenye ripoti ya CAG wajitafakari kabla ya mamlaka ya uteuzi kuchukua hatua.
Imetarayarishwa na Amri Ramadhani, Sauti ya Amerika, Dar es Salaam.
Forum