Siku moja baada ya mswaada wa sheria ya bima ya afya kupitishwa na bunge la Tanzania, wadau hao wa afya wamezitaka mamlaka husika kuangalia upya kipengele cha sheria kinachowawajibisha wale watakaoshindwa kulipia bima hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu.
Akielezea wasiwasi wake kuhusiana na mswaada huo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Nassoro Kitunda amesema kuwa matabaka yataendelea katika bima ya afya, na sheria haielezi kwa upana ni kwa namna gani bima hiyo itayaondoa matabaka hayo.
“Bima iliyopo hivi sasa ina changamoto, unaweza ukachangia bima lakini ukienda kutibiwa unaambiwa baadhi ya magonjwa hayatibiwi na bima uliyolipia” alisema Kitunda, na kuongeza “changamoto hii itaendelea kwenye huu mfumo mpya ikiwa sheria haitaelezea kwa upana ni kwa namna gani bima ya afya kwa wote itatoa huduma ya kutibu kila ugonjwa bila mashariti wala vigezo.”
Alipokuwa akiwasilisha mswaada huo bungeni Waziri wa afya Ummy Mwalimu alisema wizara inapendekeza kuwepo kwa adhabu ndogo ya asilimia kumi ya mchango wa kila mwaka kwa mtu atakayeshindwa kujiunga na bima ya afya kwa kipindi cha miaka mitatu tangu sheria itakapoanza kufanya kazi.
Suala ambalo mkurugenzi mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali la Women for self Initiative, linaloshughulikia utawala bora, msaada wa kisheria pamoja na ufuatiliaji wa rasilimali za umma kwenye sekta ya afya, Bernadetha Choma amesema, kutokana na mazingira ya uchumi, siyo kila Mtanzania atakuwa na uwezo wa kujiunga na bima ya afya, hivyo si suluhisho sahihi bali ni kutoa adhabu kwa wananchi watakaoshindwa kujiunga na bima hiyo.
“Kutokana na mazingira yetu ya Kitanzania sio kila mtu atakuwa na uwezo wa kukata hiyo bima ikiwa maisha yake ya kawaida na kipato chake hata kule kukidhi mahitaji ya kila siku, bado ni changamoto kwahiyo bado tunaona sio suluhisho kumpa adhabu mwananchi ambaye hana kipato na vipato havilingani.” alisema Choma.
Hata hivyo wananchi wameitaka serikali kuweka mfumo utakaowasaidia kupata huduma na matibabu mazuri bila kuwepo kwa changamoto yoyote pamoja na kuweka watumishi madhubuti ili wananchi wapate huduma bora ya afya
Akizungumza na Sauti ya Amerika, Ismaili Masudi ambaye ni mkazi wa jiji la Dar Es Salaam alisema “watengeneze mfumo ambao mwananchi atapata matibabu mazuri, kwa wakati bila ukiritimba,” na kuongeza “kwahiyo serikali iweke watu madhubuti kwenye eneo hilo ili wananchi wapate kile ambacho serikali itoe wanachotaka kuwatendea wananchi wake.”
Pia waziri Ummy ameainisha vyanzo vya mapato mbalimbali vitakavyotumika kugharamia watu wasiojiweza zikiwemo bidhaa za vipodozi, pombe kali na michezo ya bahati nasibu.
Habari hii imeandariwa na Amri Ramadhani, Sauti ya Amerika, Dar es Salaam.
Forum