Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 22, 2024 Local time: 22:38

Mpango wa Tanzania wa kuwahamisha wafugaji kutoka hifadhi ya Ngorongoro wakosolewa


Vijana wa Kimasai wakiendesha baiskeli zao huko Arusha.
Picha na ALEXANDER JOE / AFP
Vijana wa Kimasai wakiendesha baiskeli zao huko Arusha. Picha na ALEXANDER JOE / AFP

Watetezi wa haki za binadamu wameukosoa mpango wa serikali ya Tanzania wa kuwahamisha jamii ya wafugaji wanaoishi katika hifadhi ya Ngorongoro bila ya kuwashirikisha wakazi wa maeneo hayo.

Wakizungumza na Sauti ya Amerika Watetezi hao wameelezea wasiwasi wao kuhusu uhamishaji huo usio wa hiari chini ya mpango wa serikali wa kuziondoa jamii za wafugaji, kutoka katika makazi yao kwenye hifadhi ya Ngorongoro na kuhamishiwa kwenye Kijiji cha Msomera kilichopo katika wilaya ya Handeni Mkoani Tanga.

Mkurugenzi wa Shirika la Uraia na Msaada wa Kisheria (CILAO) Odero Odero amesema serikali ilipaswa kuwashirikisha wakazi wa Ngorongoro na jamii za wafugaji kupitia serikali zao za vijiji ili watoe maoni yao kabla ya mpango huo wa kuwahamisha wafugaji hao haujapitishwa.

Wanawake wa kimasai huko Monduli, Arusha
Wanawake wa kimasai huko Monduli, Arusha

“Kupitia mikutano ya vijiji watu wa Ngorongoro wangeshirikishwa na wangetoa mapendekezo ya nini kifanyike kama ilivyofanyika mwaka 2022” alisema Odero “wananchi hao walipokwenda kukutana na Waziri Mkuu jijini Dodoma na kupeleka mapendekezo yao ya namna bora ya kutatua changamoto za Ngorongoro.” Aliongeza.

Naye Laitayo Laiza mkazi wa Ngorongoro amesema kuwa ukosefu wa huduma muhimu katika eneo hilo kwa muda wa miaka miwili anawasiwasi kuwa ni mbinu ya kutaka kuwaondoa katika makazi yao.

Amesema kuwa “Hakuna hiyari pale kama tu watu tumenyimwa huduma za kijamii kuanzia mwaka 2020 hakuna huduma yoyote ya jamii ambayo tunapata” Laitayo alitoa mfano kwa kusema “kwa mfano miradi ya maendeleo, shule, hospitali na miundombinu mingine kama ya barabara isipokuwa zile barabara ambazo tu zina manufaa kwa shirika la utalii.”

Kulingana na msemaji Mkuu wa Serikali ya tarafa, Ngorongoro ina jumla ya kata 11 na vijiji 25 vikiwa na watu 115,000, na kuna jumla ya kaya 21,000 zinazochukua eneo la kilomita za mraba 3,700 kati ya kilomita za mraba 8,292 za eneo lote la hifadhi.

Kundi la Wanasai huko Sekenani, Juni 10, 2023. Picha na Luis Tato / AFP.
Kundi la Wanasai huko Sekenani, Juni 10, 2023. Picha na Luis Tato / AFP.

Mobhare Matinyi ambaye ni Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania ameiambia Sauti ya Amerika kuwa sababu za kuhamishwa kwa jamii hiyo ya wafugaji ni kutaka kuiendeleza na kuzuia uharibifu wa hifadhi hiyo inayokabiliwa na ongezeko kubwa la watu na mifugo.

Matinyi imeeleza sababu nyingine za uhamishaji huo ni pamoja na kuendeleza shughuli za kiuchumi kupitia utalii pamoja na maendeleo ya watu wa jamii ya wafugaji.

Alisema “Sababu kubwa ya serikali kutaka kuwahamisha wananchi hawa ni kujaribu kufikia malengo matatu, moja kuendeleza uhifadhi wa eneo la Ngorongoro la pili ni kuhakikisha kwamba shughuli za kiuchumi za fahari ya nchi yetu ya utalii zinaendelea na sababu ya tatu ni maendeleo ya watu wa jamii wanaoishi pale.”

Matinyi ameihakikishia jamii ya wafugaji wanaoishi Ngorongoro kuwa hakutakuwa na matumizi ya nguvu kwa mwananchi yoyote ambaye hatakuwa tayari kuhama katika eneo lake na badala yake serikali itaendelea kutoa elimu ya umuhimu wa kuhama katika maeneo hayo.

Imatayarishwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Dar es Salaam

Forum

XS
SM
MD
LG