Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 28, 2024 Local time: 13:43

Tanzania yaombwa kuwaelimisha wanawake wajasiriamali


Mkazi wa Zanzibar Adelisi akiwa katika shamba la mwani. Picha na AFP
Mkazi wa Zanzibar Adelisi akiwa katika shamba la mwani. Picha na AFP

Wanawake wa Tanzania wameitaka serikali kutoa elimu ya fursa mbalimbali za kiuchumi ili kuwawezesha wanawake kujikimu kiuchumi, na kuwasihi wanawake kutumia vipaji vyao wakati wakikabiliwa na changamoto mbalimbali.

Wakizungumza na Sauti ya Amerika kuhusu maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, wanawake hao wamelalamikia ukosefu wa elimu kuwa unawakwamisha wanawake wengi katika maendeleo.

Rehema Mkoha, mjasiriamali kutoka Karagwe, ameiambia Sauti ya Amerika kuwa, serikali inapaswa kutoa elimu kuhusu uwepo wa fursa mbalimbali za serikali zinazotolewa kwa ajili ya wanawake kukabiliana na changamoto zao, fursa ambazo wengi wao hawazitambui.

“Serikali ingewekeza kwenye fursa mbalimbali ambazo zinajitokeza, kuna fursa za serikali ambazo tunaziona kwenye halmashauri. Kuna fedha kwa makundi matatu: wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu. Lakini wangapi wanatambua kwamba kuna uwezekano wa kupata pesa ile ili waweze kuitumia? Hata ukishatoa elimu, bado kuna jukumu la kuwaelekeza fursa zilipo,” amesema Mkoha.

Wanawake hao pia wameitaka serikali kuongeza uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo elimu na mafunzo, upatikanaji wa mitaji, kupambana na ubaguzi na ukatili, teknolojia na ubunifu, pamoja na kuimarisha miundombinu katika maeneo ya vijijini ikiwemo umeme, maji, na miundombinu mingine ya kiuchumi.

Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino, Dkt. Anne Gongwe, amesisitiza kuwa serikali inapaswa kutengeneza mifumo bora ya usimamizi wa uwekezaji kwa ajili ya kuwakomboa wanawake.

Amesema “Kama serikali kweli inataka kumkomboa mwanamke, inatakiwa iwe makini katika uwekezaji inaofanya.”

“Iwe makini katika kuangalia kweli hizo hela zinatolewa, wanawake wanapata. Kuwe na uangalizi wa makini ili kusiwe na uchakachuaji, wanawake wawe walengwa wapate hela zao na wasaidiwe vile vile.” Aliongeza

Naye, Glori Akida, mkurugenzi wa kampuni ya C&G (T) Ltd, amewataka wanawake kutokata tamaa wanapokutana na changamoto mbalimbali, na kuwasihi kuendeleza vipawa walivyonavyo ili viweze kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.

“Watakutana na changamoto, wasikate tamaa. Kipaji chao walichowekewa wanatakiwa wakisimamie na wakiendeleze. Kila mtu ana kitu ambacho Mungu amemuwekea ndani yake. Tunatakiwa tusimame imara kuweza kusimamia vipaji vyetu na kuhakikisha tunasonga mbele. Tusikatishwe tamaa wala tusirudi nyuma,” alisema Akida

Kaulimbiu ya mwaka huu inasema 'Wekeza kwa wanawake: Kuharakisha maendeleo', ikihimiza hatua za dhati kuelekea kujenga jamii inayowaheshimu wanawake, kuondoa vikwazo vinavyowakabili, na kuwapa wanawake nafasi ya kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Imetayarishwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Dar es Salaam

Forum

XS
SM
MD
LG