Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 29, 2025 Local time: 02:33

Ruto awataka wabunge wa Afrika Mashariki kuimarisha ushirikiano na kuboresha maendeleo


Rais Ruto akihutubia kikao maalumu cha bunge la Afrika Mashariki
Rais Ruto akihutubia kikao maalumu cha bunge la Afrika Mashariki

Rais wa Kenya William Ruto amelitaka bunge la Afrika Mashariki kuendelea kuwa kiungo muhimu katika juhudi za kuimarisha ushirikiano na watu wa Afrika Mashariki na mshikamano wa nchi wanachama ili kuboresha maendeleo ya kijamii na kiuchumi ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.

Akihutubia Kikao Maalum cha Bunge hilo jijini Nairobi, amewataka Wabunge wa jumuiya hiyo kutekeleza majukumu na sera zinazohimiza mshikamano wa kikanda katika kiini cha kutunga sera za nchi binafsi na kuhakikisha EAC inawakilisha, na kutekeleza maslahi ya nchi wanachama.

Kikao hicho cha tatu cha bunge hilo lenye makao yake makuu Arusha,Tanzania, Rais Ruto amewaeleza wabunge hao kukabiliana na changamoto za ukuaji wa biashara na uwekezaji kama vile vizuizi visivyo vya ushuru, migogoro ya kibiashara inayosumbua na yenye gharama kubwa, kanuni zinazokinzana za kodi, utekelezaji dhaifu na uhaba wa rasilimali, pamoja na ushiriki mdogo wa sekta binafsi.

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inajumuisha mataifa nane ya Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na Somalia, kwa misingi ya kupanua na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi wanachama katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kitamaduni, utafiti na teknolojia, ulinzi, usalama kwa faida ya nchi wanachama.

Wabunge wa bunge la Afrika Mashariki
Wabunge wa bunge la Afrika Mashariki

Bunge hilo linatakiwa kubuni sera zinazowezesha soko huria kwa kupunguza vikwazo vya ushuru na visivyo vya ushuru na kurahihisha taratibu za forodha na vile vile kuweka misingi ya soko la pamoja, umoja wa kifedha na shirikisho la kisiasa, anavyoeleza Ben Omillo, mfuatiliaji wa masuala ya bunge hilo.

Wabunge wa EALA wanahudhuria vikao vya bunge hilo vya mwezi mzima jijini Nairobi, kwa kuzingatia Kifungu cha 55 cha Mkataba wa kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambacho kinatoa masharti ya vikao vya mzunguko vya Bunge kati ya nchi wanachama, na rais Ruto aliyeongoza ufunguzi rasmi wa kikao cha 3 cha mkutano wa 3 wa Bunge la 5 la Bunge la Afrika Mashariki, amesema kuwa bunge hilo limetwikwa jukumu la kuweka sera na mikakati bora ambayo inachangia harakati za umoja za kuleta mabadiliko chanya katika siasa na uchumi, kijamii na kitamaduni, utafiti na maendeleo pamoja na teknolojia na uvumbuzi, ulinzi na usalama kwa wa watu wa Afrika Mashariki.

Ikiwa na Pato la Taifa la dola bilioni 350, na idadi ya watu milioni 350, Ruto ameeleza kuwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kivutio cha uwekezaji. Hata hivyo, Bw Omillo anaeleza kuwa bunge hilo linahitaji kuwa sehemu ya uidhinishaji wa sera zinazoiwezesha jumuiya hiyo kufikia uwezo na malengo yake kwa manufaa ya watu wa nchi wanachama.

Bunge hilo kupitia vikao vyake vya Nairobi, linalenga kujadili sheria zinazopendekezwa kwa uwianishaji, na mikakati ya kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, Sauti ya Amerika, Nairobi

Forum

XS
SM
MD
LG