Thunberg : Wanasiasa miaka 30 bila maamuzi au wanafunzi kukosa masomo saa kadhaa?

Wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali wakiandamana mjini New Delhi, India, Machi 15, 2019.

Wanafunzi kutoka takriban mataifa 40 wamesitisha masomo kuitikia wito wa mwanafunzi mwenzao aliyewataka kupaza sauti zao kuhamasisha hatua zichukuliwe kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Vuguvugu hilo la kutetea usafi wa mazingira ulianza ulaya na kuenea kote duniani tangu mwaka 2018.

Wanafunzi wakosolewa

Ingawa hatua ya wanafunzi inapongezwa na wengi, lakini wengine wanahoji iwapo kunaulazima wowote kwa wanafunzi kusitisha masomo kwa ajili ya kushughulikia masuala ya kisaisa.

Wanasiasa wa kihafidhina hata hivyo hawaja kubali bado kuna mabadiliko ya hali ya hewa na Waziri Mkuu wa Australia Scott Morrion alieleza upinzani wake mwezi Novemba mwaka 2018 juu ya wanafunzi kuacha masomo na kuandamana.

Waziri Mkuu wa Australia amesema: "Watoto inawalazimu kuwa shuleni. Hatuungi mkono wazo la watoto kutokwenda shule ili kushiriki katika mambo yanayoweza kushughulikiwa nje ya wakati wa masomo."

Udhaifu wa wanasiasa

Greta Thunberg amewajibu kwa ujumbe wa tweeter akisema "wanasiasa wamepoteza miaka 30 ya kutochukuwa hatua na hiyo ni mbaya zaidi kuliko kukosa masomo ya saa kadhaa."

Wanafunzi katika baadhi ya nchi za ulaya kwa miezi kadhaa sasa wamekuwa wakigoma kuingia madarasani kila siku ya ijumaa tangu mwezi Agosti 2018, pale mwanafunzi kutoka Sweden Greta Thunberg mwenye umri wa miaka 15 kuacha kwenda darasani na badala yake kwenda kukaa mbele ya bunge la Sweden kuwataka wabunge kuchukuwe hatua za haraka kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Tangu siku hiyo maelfu kwa maelfu ya wanafunzi wa Ujerumani, Sweden, Uingereza na hadi Australia wamefuata mfano wa Thunberg na kuacha masomo kumuunga mkono na kuanzisha vuguvugu la kutetea mazingira lakini Greta anasema yeye hakuanzisha vuguvugu hilo.

Greta Thunberg, Mtetezi usafi Mazingira kutoka Sweden,

Sidhani nimeanzisha vuguvugu . ninadhani kwamba nilichukuwa hatua tu wakati ambapo watu zaidi na zaidi wanaanza kufahamu hali tunaoishi hivi sasa na pia kuwaonyesha watu mbinu unaoweza kutumia sauti yako isikike.

Kwa hakika ni vuguvugu linaloleta mafanikio kwani mwezi uliyopita Thunberg alipata ahadi kutoka Umoja wa Ulaya wa kuwezesha kutumia mabilioni ya fedha kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Sasa mwanafunzi huyo aliyegeuka kuwa mwanaharakati alipata umashuhuri kupitia mitandao ya kijami akianzisha hashtag school strike for climate na Friday forfuture iliyomsababisha kualikwa kwanza kuzungumza kwenye mkutano wa viongozi wa Jopo la uchumi duniani mjini Davos mwaka 2018.

Katika hotuba yake Thunberg alitoa ujumbe wa wazi kuwa : Ninataka muingiwe na taharuki. Ninataka muhisi hofu ninayohisi mimi kila siku. Na halafu ninawataka muchukuwe hatua."

Wito wake unaungwa mkono sasa na vijana na wanafunzi pamoja na walimu katika kila pembe ya duniahapo jana wanafunzi wa Hong Kong na japan walitangaza wanaungana na juhudi hizo.

Wakati huohuo wanafunzi wa Ujerumani na Ufaransa Ijumaa wanaandamana wakishinikiza wanasiasa na viongozi wachukuwe hatua kudhibiti uchafuzi wa mazingira.

Athari za uharibifu wa mazingira

Wachambuzi wa masuala ya mazingira wanasema kuwa ikiwa serikali hazitafanya kitu chochote, dunia itakuwa mahala pabaya zaidi kuishi kwa sababu kutakuwa na vimbunga vikali, ukame, mafuriko vita vya kupigania rasilmali kwa hivyo hakutakuwa na utulivu duniani.

Vugu vugu hili limepata uungwaji mkono wa rais wa Kamisheni ya Ulaya Jean Claude Juncker, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na wanasiasa wengine mashuhuri walovutiwa kuona sauti ya wanafunzi zinaleta mabadiliko.