Wananchi wa Algeria washeherekea kujiuzulu kwa Bouteflika

Wananchi wa Algeria washeherekea kujiuzulu kwa Rais Abdelaziz Bouteflika April 2, 2019, Algiers.

Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria, 82, amewasilisha barua ya kujiuzulu siku ambayo maandamano makubwa yakiendelea dhidi yake. Bouteflika amekuwa katika madaraka kwa kipindi cha miaka 20.

Wakati huohuo magari yalikuwa yakipiga honi katikati ya jiji la Algiers na mara watu walionekana wakitoka majumbani wamebeba na kupeperusha bendera za Algeria kwa shangwe na vifijo kufuatia kujiuzulu kwa Bouteflika.

Televisheni ya Taifa imeripoti kuwa Bouteflika aliliambia rasmi baraza la katiba hatua ya kuhitimisha utawala wake.

Shirika la habari la serikali APS la nchi hiyo lilipata nakala ya barua yake ya kujiuzulu na limenukuu kauli ya Bouteflika akisema kuachia madaraka kwake kutatoa nafasi kwa Algeria kupata maendeleao na kuwa na mustakabali mwema.

Algeria kwa sasa inapitia kipindi cha mpito, mara baada ya rais huyo kujiuzulu, na kuna swali ni nini kitajiri katika taifa hili lenye utajiri wa gesi na mshirika wa nchi za Magharibi katika vita dhidi ya ugaidi.

Baraza la kikatiba lenye wanachama 12 nchini Algeria linatarajiwa kufanya kikao chake Jumatano kuthibitisha hatua ya kujiuzulu kwa Bouteflika.

Televisheni ya taifa ilimuonyesha kiongozi huyo ambaye ni mgonjwa akimkabidhi barua yake ya kujiuzulu rasmi kwa rais wa baraza hilo Tayeb Belaiz.

Kwa mujibu wa Katiba ya Algeria rais akiaga dunia au kujiuzulu baraza la katiba ni lazima lithibitishe, kabla ya mabunge yote mawili kukutana na spika wa bunge kuteuliwa kama rais wa mpito kwa siku 90, huku maandalizi ya uchaguzi wa rais yakifanyika. Hivyo basi Abdelkader Bensalah, 77, mshirika wa Bouteflika ambaye ni spika wa bunge la sasa nchini Algeria, atakuwa ni rais wa mpito.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amesema Marekani inaipongeza hatua ya Bouteflika kujiuzulu na imesema kuwa sasa mustakbali wa Algeria uko mikononi mwa wananchi wenyewe.

Naye Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amesema hatua ya rais Bouteflika inafungua ukurasa mpya na muhimu katika historia ya Algeria.

Rais huyo wa zamani anadaiwa kuwa alikuwa ananang'ang'ania madaraka, ambapo kabla ya kujiuzulu alikumbana na shinikizo kubwa aachie madaraka pale alipochukua hatua kuwania muhula wa tano madarakani licha ya kutoonekana hadharani baada ya kupatwa nakiharusi mwaka 2013.