Wanajeshi Mali waahidi kurejesha utulivu na kusimamia kipindi cha Uchaguzi

Wanajeshi wa Mali wakishangiliwa walipowasili katika uwanja wa Independence Square mjini Bamako, Mali on August 18, 2020.

Wanajeshi waliomuondoa madarakani rais wa Mali, na serikali yake katika mapinduzi ya kijeshi ambayo yamelaaniwa nje ya nchi Jumatano wameahidi kurejesha utulivu, na kusimamia kipindi cha mpito mpaka uchaguzi utakapofanyika.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters wanajeshi hao wamesisitiza kuwa uchaguzi huo utafanyika katika wakati muwafaka.

Wakati huohuo Rais Ibrahim Boubacar Keita alijiuzulu, na kuvunja bunge Jumanne jioni saa kadhaa baada ya kuwekwa kizuizini na jeshi.

Taifa la Mali linakabiliwa na wanamgambo wenye msimamo mkali, na maandamano makubwa yaliozua mzozo wa nchini humo.

Hata hivyo haikuweza kufahamika mpaka sasa juu ya ni nani kwa sasa anatawala katika nchi hiyo.

Lakini msemaji wa wanajeshi waliotekeleza mapinduzi hayo, wanaojiita kamati ya kitaifa ya uokozi wa wananchi, amesema walifanya hivyo kuiokoa Mali isiingie katika mzozo mkubwa zaidi.

Mapinduzi hayo yalikosolewa muda mfupi tu baada ya kufanyika hapo jana na washirika wa kikanda na kimataifa, ambao wanaona kuanguka kwa utawala wa Keita kutazorotesha amani katika nchi hiyo iliyokuwa koloni la Ufaransa, na eneo zima la Afrika Magharibi la Sahel.