Chauvin ameshtakiwa katika kesi ya mauaji ya Mmarekani Mweusi George Floyd, karibu mwaka mmoja uliopita.
Baada ya kusikia hoja za kufunga kesi hiyo Jumatatu, baraza la mahakama la watu 12 - wakiwemo wazungu sita na watu sita ambao ni weusi au wa jamii nyingine – walichukua saa chache tu kujadili kesi hiyo iliyochukua wiki tatu, kabla ya kufikia uamuzi.
Rais wa Marekani, Joe Biden, na makamu wake Kamala Harris, walielezea kuridhika kwao na uamuzi huo, na kusema kwamba huu ndio wakati wa kupitisha sheria ambazo zinahakikisha usawa katika mfumo wa sheria za Marekani.
Hukumu katika kesi hiyo itafanyika katika miezi miwili, jaji aliyeisimamia amesema. Tangu kesi hiyo ianze, umati wa watu walikuwa wamekusanyika karibu na Kituo cha Serikali cha Kaunti ya Hennepin, ambapo kesi hiyo ilifanyika, na mahali ambapo Floyd alikufa. Walishangilia wakati uamuzi ulipotangazwa.