Wahamiaji watoto wanachukuliwa kama watu wazima Uhispania

Wahamiaji walipowasili kwa boti ya mbao kwenye Kisiwa cha Canary cha El Hierro

Ongezeko la idadi ya wahamiaji wanaofanya safari hatari kutoka Afrika Magharibi kwenda Visiwa vya Canary vya Uhispania linaleta shida kwa mamlaka za kieneo.

Wakati mashirika ya haki za binadamu yakionya kwamba watoto wengi wahamaiaji wanachukuliwa kimakosa kama watu wazima na polisi wa Uhispania, jambo linalowaweka katika hatari zaidi.

Mpaka sasa mwaka huu, zaidi ya wahamiaji 32,000 wamewasili katika Visiwa vya Canary kutoka Afrika Magharibi - idadi kubwa zaidi tangu 2006.

Moussa Camara mwenye umri wa miaka 15 alikuwa yatima kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2021 katika nchi yake ya Guinea. Alichagua kutoroka, akitumia siku 11 baharini ndani ya mashua ya mbao katika safari hatari kutoka Senegal kwenda kisiwa cha Uhispania cha Tenerife, akiwa pamoja na wahamiaji wengine 240. Nusu ya muda huo, hakuwa na chakula au maji.

Watu 20 walikufa wakati walipokuwa wakijaribu kuvuka, amesema, miili yao ilitupwa kando ya mashua.

Akiwa na vidonda kutokana na kupigwa na jua, njaa na ukosefu wa maji mwilini, hatimaye Camara alifika Tenerife Oktoba 27, 2021.

Lakini mateso yake hayajaisha. Mamlaka ya Uhispania walitaja Camara na rafiki yake kuwa ni watu wazima badala ya watoto, ikimaanisha kuwa hawakuruhusiwa kukaa katika kituo cha watoto au kupata fursa bora zinazopatikana kwa wale walio chini ya miaka 18.

"Katika kituo, tulisema tuna umri wa miaka kumi na tano. Lakini hawakuandika hivyo - walituchukua kama watu wazima. Lakini sisi ni watoto, sisi ni watoto - hivyo walituleta hapa. Walileta karatasi zetu. Walitusaliti," Camara aliliambia shirika la Reuters.

Polisi wa Uhispania waliwapeleka wavulana hao wawili Las Raices, kambi ya zamani ya kijeshi katika milima ya Tenerife, ambapo wahamiaji watu wazima wapatao 2,000 wanasubiri kuhamishwa kwenda bara huko Uhispania.