Rais wa Marekani Joe Biden atawakaribisha viongozi kutoka Amerika Kusini na Caribbean huko White House siku ya Ijumaa kujadili masuala ya kiuchumi na uhamiaji wakati akijaribu kuimarisha uhusiano katika eneo hilo ili kukabiliana na China na washindani wengine wa kimataifa.
Viongozi kutoka Barbados, Canada, Chile, Colombia, Costa Rica, Jamhuri ya Dominika, Ecuador, Peru na Uruguay wanatarajiwa kuhudhuria mkutano wa Ijumaa pamoja na wawakilishi kutoka Mexico na Panama.
Mkutano wa Viongozi wa Ushirikiano wa Marekani kwa Ustawi wa Kiuchumi (APEC) unakuja wakati ajenda ya sera za mambo ya nje ya Biden zikitawaliwa na mzozo wa Israel na Hamas huko Gaza na azma ya Ukraine ya kuwafukuza wavamizi wa Russia.
Marekani itatangaza zana mpya za kiuchumi pamoja na Benki ya Maendeleo ya Marekani na wafadhili binafsi kwa nchi zinazopokea wahamiaji katika Ukanda wa Magharibi-Western Hemisphere kwa lengo la kuongeza ushirikiano wa kiuchumi na kuzuia kuwasili kwa wahamiaji kwenye mpaka wa Marekani na Mexico, maafisa waandamizi wa utawala walisema.
“Wakati nchi zinafanya kazi pamoja kwa ajenda ya pamoja ya kiuchumi ina uwezo wa kubadilisha kwa kiasi kikubwa mienendo ya kiuchumi kwenye eneo ambalo limekuwa na kasi ya polepole kuliko wengine katika kuikubali teknolojia kwa kuchukua fursa ya mwelekeo wa karibu” afisa mwandamizi katika utawala alisema.
Biden ana imani kwamba uwekezaji unaolengwa wa kiuchumi katika nchi zinazohifadhi wakimbizi na wahamiaji “ni muhimu katika kuleta utulivu wa uhamiaji” afisa mwingine wa pili aliongeza.
Nchi sita za APEC ambazo ni Costa Rica, Ecuador, Colombia, Peru, Chile na Panama zilitoa hadhi ya kisheria kwa mamilioni ya watu waliokimbia makaazi yao huko Western Hemisphere, afisa huyo alieleza.
Forum