Tuhuma dhidi ya Bashir na maafisa wengine watatu waliokuwa katika serikali yake, ni pamoja na kuhusishwa na mauaji ya halaiki na uhalifu wa vita walioufanya huko Darfur.
Mauaji hayo yalitokea baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kuzuka mwaka 2003. Lakini maafisa wa serikali ya Sudan wamegusia kuwa kesi hiyo huenda isisikilizwe The Hague.
Mohamed Eisa alikuwa na umri wa miaka 12 pale wanamgambo waliposhambulia kijiji chake upande wa Mashariki mwa Darfur miaka 10 iliyopita, na baba yake na ndugu zake kuuawa, na kuwalazimisha familia yote kukimbia kuokoa maisha yao.
Kijana huyu amekuwa akiishi katika muongo mmoja upande wa Magharibi ya Sudan kwenye kambi ya Kalma, kambi kubwa kuliko zote katika eneo la Darfur ikiwahifadhi wale waliolazimika kukimbia makazi yao, ikiwa na wakazi takriban nusu milioni.
Kama ilivyo kwa waathirika wengi wa vita katika eneo la Darfur, Eisa anailaumu serikali ya rais wa zamani Omar al-Bashir kuhusika na vita hivyo, ambavyo Umoja wa Mataifa wanasema imesababisha watu takriban 300,000 kuuawa na watu milioni 2.5 kulazimika kuyakimbia makazi yao tangu mwaka 2003.