Tsega Fitsum ni mwalimu wa kujitolea katika shule ya Mai Weyni iliyoko katika mji mkuu wa mkoa wa Tigray, Mekelle. Amesema shule zilipofunguliwa tena mara tu baada ya mapigano kusitishwa mwezi Novemba mwaka jana, mawazo ya wanafunzi wake bado yamejikita kwenye mzozo huo.
"Walikuwa wanapendelea zaidi kuchora bunduki badala ya kuandika alfabeti na namba," mwalimu huyo aliiambia VOA. " lakini kwa sasa tunasema vita vimekwisha, kuna amani na hakuna hofu, na wanafunzi wanapaswa kufanya kazi kwa uhuru.' Wakati tukiwaambia hivyo, wanaanza kuandika namba na alfabeti."
Pamoja na kwamba ishara hiyo ni nzuri, hakika madhara ya vita yatakuwepo kwa miaka mingi ijayo. Shule hiyo ya Mai Weyni ipo kwenye makazi ya watu zaidi ya 8,500 ambao walikimbia makazi yao kwa sababu ya vita. Watoto zaidi ya 5,100 walio na umri wa miaka chini ya 18, wengi wao wakiwa wamenyimwa fursa ya masomo kwa zaidi ya miaka miwili.
Vita kati ya serikali ya Ethiopia na vikosi vya Tigray vimewaacha watoto wengi kuwa yatima au kutengana na familia zao. Wataalam wanasema hisia zenye majeraha zinaendelea kuwaathiri watoto hao, wakati changamoto za kuliponya taifa hilo lililokumbwa na vita zikianza.
Mekelle ilikuwa eneo la mashambulizi ya anga ya serikali ya Ethiopia, mashambulizi yaliyo athiri maeneo yakiwemo yale ya uwanja wa michezo wa shule ya chekechea. Mkazi mmoja wa Mekelle, Gebregziabher Hadush, alisema kiwewe kilichosababishwa na mashambulizi hayo ya anga bado kipo kwenye hisia za watu.
Kulingana na ripoti ya mwaka 2022 ya Umoja wa Mataifa, watoto milioni 1.39 katika mkoa wa Tigray hawakuhudhuria masomo kwa sababu ya vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe vya Ethiopia.