Viongozi wa upinzani waitisha maandamano upya Khartoum

Susana Abdalla Hassan, mfanyakazi wa Benki ya Khartoum, akishikilia bango lenye kuunga mkono mapinduzi wakati wakifanya mgomo nje ya soko la bidhaa la Al-Waha mall, Khartoum, Sudan, Mei 28, 2019.

Maelfu ya waandamanaji walikusanyika nje ya makao makuu ya jeshi la Sudan huko Khartoum Alhamisi wakishinikiza jeshi kukabidhi madaraka kwa raia.

Hatua hiyo inafuatia wito wa viongozi wa upinzani kwa waandamanaji washiriki maandamano mengine makubwa kuwashinikiza majenerali wa jeshi kuharakisha mchakato wa kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia.

Huku wakiimba nyimbo za kuunga mkono serikali ya kiraia na wakipepea bendera za Sudan, waandamanaji hao ambao wengi wao ni vijana waliungana na wenzao kwa kukaa nje ya makao makuu ya jeshi hilo wakati giza lilipoingia.

Eneo hilo ndio limekuwa sehemu kuu ya vuguvugu la maandamano yaliomtoa madarakani kiongozi wa muda mrefu Omar al -Bashir, mwezi Aprili 2019, na kutaka majenerali wa jeshi waliochukua nafasi yake kukabidhi madaraka kwa raia.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.