Viongozi wa APEC wakutana bila ya Trump

Rais wa China Xi Jinping

Viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Asia na Pacific, APEC, wameanza kuwasili katika mji wa Port Moresby , kisiwani Papua New Guinea kwa mkutano wa siku mbili ambao Rais wa Marekani Donald Trump hatahudhuria kutokana hasa na mvutano wake wa kibiashara na China.

Rais wa China Xi Jingping aliwasili huko tangu Alhamisi kuanza ziara rasmi ya siku mbili ya kwanza kufanywa na kiongozxi wa China nchini humo.

Kiongozi huyo alitangaza misaada mbali mbali kwa nchi hiyo, ikiwa ni pamoja na kufungua barabara kuu iliyogharimiwa na China.

Alitangaza pia msaada kwa nchi za Asia katika kile wachambuzi wanakieleza ni juhudi za China kuchukua nafasi ya Marekani kutokana na sera za Rais Trump kujiondowa kutoka mikataba ya kimataifa.

Rais Xi ameahidi msaada mkubwa kwa Papua New Guinea taifa maskini kabisa katika kanda hiyo ya kusini mashariki ya Asia na alikutana na viongozi wa biashara wa visiwa vya bahari ya Pacific hapo jana.

Mawaziri wa biashara wa APEC wamekuwa wakikutana kabla ya mkutano wa viongozi kesho na wameshindwa kufikia makubaliano juu ya tangazo la pamoja kutokana na mvutano juu ya mageuzi katika shirika la biashara dunia, WTO.

Kulingana na ajenda ya mkutano mazungumzo yatazingatia juu ya upanuzi wa ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda na kuimarisha miundo mbinu ya kidijitali.