Mkutano huo unaofanyka jijini Nairobi unahudhriwa na marais wa nchi tano za Afrika akiwemo Hakainde Hichilema wa Zambia, Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe, Nangolo Mbumba wa Namibia, Dkt Lazarus Chakwera wa Malawi na Faustin-Archange Touadéra wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, pamoja na mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat.
Katika mktano huo rais Hichilema wa Zambia amesema inastaajabisha kuwa mataifa mengi ya Afrika bado yanaendelea kuagiza kwa wingi mbolea kutoka mataifa ya nje licha ya uwezo wake wa kujitegemea kuzalisha chakula cha kutosha, na kutoa wito kwa mataifa ya Afrika kufanya biashara kwa pamoja ikiwa ni sehemu ya kuinua uwezo wa nchi husika katika uzalishaji wa chakula.
Rais wa Kenya William Ruto ameeleza kuwa ni sharti Afrika ijitahidi kupata mbolea ya bei nafuu, bora na inayoweza kupatikana kwa urahisi kwa utengenezaji wa ndani ya mataifa ya Afrika, hatua ambayo itaongeza tija na uzalishaj na kufanya Afrika ijitosheleze kwa chajula.
Aidha Ruto amewataka wakuu hao wa nchi kuchuku jukumu la kulibadilisha bara la Afrika kutoka hali ya njaa hadi kuwa kapu la chakula la kimataifa linalojitosheleza.
Hata hivyo Moussa Faki Mahamat, amesema kuwa kuna baadhi ya nchi za Afrika huzalisha mbolea lakini bado Afrika inategemea zaidi mbolea kutoka nje, ambayo ni ghali kwa wakulima , mbali na kuwa Afrika kuwa kituo chake cha ukuzaji wa mbolea nchini Zimbabwelkilichoanzishwa mwaka 1982.
Kongamano hili la siku tatu ambalo limekamilika Alhamisi, baada ya mashauriano ya kujaribu kutafuta njia bunifu, na mikakati ya kukuza ubora wa udongo wenye rotuba na mbolea kwa ajili ya kuboresha kilimo endelevu barani Afrika ili kumaliza njaa, utapiamlo na umaskini, limeafikia kuwa mataifa ya Afrika yatashirikiana katika uwekezaji ili kuendesha sera, fedha, utafiti na maendeleo, masoko, na kujenga uwezo kwa ajili ya mbolea na usimamizi endelevu wa afya ya udongo barani Afrika.
Vile vile, limeafikia kuongeza uzalishaji wa ndani na usambazaji wa mbolea mara tatu, kuhakikisha inawafikia asilimia 70 ya wakulima wadogo katika bara zima na vile vile kuongeza upatikanaji na uwezo wa kumudu mbolea kwa wakulima wadogo, kukuza ufanisi zaidi na matumizi endelevu ya mbolea.
Pia, wadau wamekubaliana kubadili uharibifu wa ardhi na kurejesha afya ya udongo kwa angalau 30% ya udongo ulioharibiwa kufikia 2033.
Na kuhusu ufadhili, wakuu wa nchi za Afrika, wameahidi kutekeleza kikamilifu mfumo wa ufadhili wa mbolea ya Afrika ili kuboresha uzalishaji, ununuzi na usambazaji wake.
Hata hivyo, Dkt Oscar Koech, mtaalam wa kilimo na Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi, anaeleza kuwa nchi za Afrika zinastahili kuwezesha upatikanaji wa mbolea ya bei nafuu na mifumo ya ukulima inayoendana na ubora wa ardhi ya Afrika kuimarisha uzalishaji wa chakula.
Aidha, Dkt Koech ameeleza kuwa ni lazima pawepo na ufahamu wa aina ya virutubisho vinavyohitajika, na kusambaza kiasi cha mbolea kinachotosheleza mahitaji husika ya wakulima wa Afrika.
Imetayarishwa na Kennedy Wandera, Sauti ya Amerika, Nairobi.