Mzozo huo uliongezeka kwa haraka Alhamisi, wakati Rais Mohamed Abdullahi Mohamed, ambaye ni maarufu kama Farmajo, aliposimamisha mamlaka ya utendaji ya Waziri Mkuu Mohamed Hussein Roble.
Kitendo hicho kilipingwa mara moja na Waziri Mkuu na kueleza kwamba kinakwenda kinyume na sheria.
Viongozi hao wawili wamekuwa wakivutana juu ya uteuzi wa maafisa wa juu wa usalama katika mzozo ambao unatishia kuhatarisha uchaguzi uliocheleweshwa mara kwa mara, na kuvuruga juhudi za kukabiliana na uasi wa Kiislam uliokuwepo kwa muda mrefu.
Viongozi wa majimbo matano huru ya Somalia waliwataka wahusika kuacha kutupiana maneno, na kutatua tofauti zao kupitia mazungumzo ya upatanishi na kuheshimu katiba ya mpito.