Huduma za intanet na simu za mkononi zilionekana zimefungwa mjini Khartoum Jumapili mapema kabla ya maandamano yaliyopangwa dhidi ya utawala wa kijeshi, mashuhuda wa Reuters walisema.
Madaraja yote yanayouunganisha mji wa Khartoum yalifungwa, shuhuda mmoja wa Reuters alieleza.
Maandamano ya Jumapili yametokea baada ya watu sita kufariki na mamia wengine kujeruhiwa katika maandamano ya nchi nzima dhidi ya utawala wa kijeshi Alhamisi. Idadi ya vifo tangu vikosi vya usalama vilipoanza msako mkali mwezi Oktoba imefikia 54, Kamati Kuu ya Madaktari wa Sudan imesema.
Jeshi lilichukua madaraka katika mapinduzi ya Oktoba 25 yaliyomaliza makubaliano ya kushirikiana madaraka na vikundi via kisiasa vya kiraia. Makubaliano ya m waka 2019 yalitakiwa kufungua njia kwa ajili ya serikali ya mpito na hatimaye kuitisha uchaguzi kufuatia kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir.
Maandamano dhidi ya utawala wa kijeshi yameendelea hata baada ya Abdalla Hamdok kurejeshwa madarakani kama waziri mkuu mwezi uliopita.
Waandamanaji wanadai kuwa jeshi lisiwe na madaraka yoyote katika serikali wakati wa kipindi cha mpito kelekea uchaguzi huru.
Baadhi ya watu walifanikiwa kuweka picha kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha maandamano katika miji kadhaa, ikiwemo Ad-Damazin na Port Sudan.
Kituo cha Televisheni cha Al Hadath kimemnukuu mshauri wa kiongozi wa kijeshi Abdel Fattah Al-Burhan akisema jeshi halitamruhusu mtu yeyote kuliingiza taifa katika machafuko na kwamba kuendelea kwa maandamano kunasababisha matatizoya ya “kimwili, kisaikoloia na kiakili kwa nchi” na “haitawezekana kufikia suluhu ya kisiasa.”
Katika matukio ya karibuni wakati mawasiliano yalipositishwa, vyanzo katika makampuni ya mawasiliano wameiambia Reuters kuwa mamlaka imeyalazimisha makampuni yanayotoa huduma kusitisha huduma zao. Maafisa hao hawakuweza kupatikana mara moja kutoa maoni yao siku ya Jumapili.
Katika hotuba yake iliyorushwa na televisheni Ijumaa, Burhan amesema mivutano juu ya madaraka na watu kupoteza maisha kunamaanisha kuwa kila mtu “atumie sauti ya busara.””
Burhan aliongeza, “Njia pekee ya kutawala ni kwa ridhaa ya umma kupitia uchaguzi.”
Baraza Huru la Sudan, ambalo linaongozwa na Burhan, Ijumaa limelaani ghasia zilizotokea wakati wa maandamano ya Alhamisi, akiongeza Baraza limeamuru mamlaka husika kuchukua hatua za kisheria na kijeshi kuzuia hilo kutokea tena na “hakuna ambaye hataadhibiwa.”
Wiki iliyopita, Baraza hilo lilirejesha amri ya kukamata na kuwaweka kuzuizini kwa vyombo vya usalama wa taifa.
Chanzo cha habari hii ni Shirika la Habari la Reuters