Upinzani Tanzania wasema bado bajeti ya maendeleo inautekelezaji duni

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakati makadirio ya bajeti ya nne ya serikali ya Tanzania ya awamu ya tano yakitarajiwa kusomwa bungeni jijini Dodoma, Alhamisi, bado takwimu rasmi zinaonyesha kuna utekelezaji duni wa bajeti ya maendeleo licha ya makusanyo ya ndani kuongezeka.

Hali hiyo inatokana na kile kilichoelezwa na serikali kwamba kiwango kikubwa cha makusanyo kinatumika kulipa Deni la Taifa na mishahara ya watumishi wa umma.

Kwa mujibu wa gazeti la Nipashe,taarifa zilizowasilishwa bungeni wakati wa Bunge la Bajeti, zinaonyesha utekelezaji wa bajeti ya maendeleo kwa miaka yote mitatu, yaani kuanzia 2016/17 uliokuwa wa bajeti ya kwanza ya serikali ya awamu ya tano hadi 2018/19, umekuwa chini ya asilimia 50 karibu kwa wizara zote, huku baadhi ya wizara zikiwa hazijapewa hata senti moja.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ilieleza bungeni wakati wa Bunge la Bajeti mwaka 2018 kuwa, kati ya mafungu yote 47 ya wizara mbalimbali yaliyostahili kupata fedha za maendeleo mwaka wa fedha 2017/18, ni mafungu 16 tu yaliyokuwa yamepata fedha kwa zaidi ya asilimia 50 hadi Machi 31, 2018.

Kamati hiyo iliweka wazi kuwa hali hiyo inatokana na kiasi kikubwa cha fedha zinazokusanywa na serikali, kutumika kulipa Deni la Taifa.

Kamati hiyo ilibainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2017/18, hadi kufikia Februari 2018, serikali ilikuwa imetumia Sh. trilioni 5.54 kulipa Deni la Taifa. Kati yake, Sh. trilioni 4.094 zilitumika kulipa madeni ya ndani na Sh. trilioni 1.446 kwa madeni ya nje.

"Kulingana na Tathmini ya Uhimilivu wa Deni, deni letu ni himilivu kwa asilimia 34.4 ukilinganisha na ukomo wa asilimia 56.

"Hata hivyo, ukilinganisha makusanyo ya ndani yanayotokana na kodi na malipo ya Deni la Taifa, utaona kuwa mpaka Desemba 2017, makusanyo ya ndani yalikuwa Sh. trilioni 7.678 na malipo ya Deni la Taifa mpaka Februari yalikuwa Sh. trilioni 5.54.

"Ni kwamba kiasi kikubwa cha makusanyo ya ndani kinakwenda kulipa Deni la Taifa," Jitu Soni, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, alisema.

Nayo Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2016/17, uliokuwa wa kwanza kwa serikali ya awamu ya tano kukaguliwa, ilionyesha malengo ya makusanyo ya serikali kwa mwaka huo wa fedha yalifikia asilimia 94, lakini fedha za miradi ya maendeleo zilizotolewa zilikuwa chini ya asilimia 50.

Akizungumza na gazeti la Nipashe kuhusu mapungufu hayo, Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, Halima Mdee, alisema kuwa ili kukabiliana na utekelezaji duni wa bajeti ya maendeleo, serikali inapaswa kuruhusu taasisi za nje kuja kufanya tathmini ya kifedha (credit rating).

Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe (Chadema), alisema anaamini kwa kuruhusu taasisi huru kufanya tathmini ya kifedha nchini, kutaisaidia Tanzania kupata mikopo yenye riba nafuu badala ya mikopo ya masharti magumu ya kibiashara inayopewa kwa sasa.

"Kwa hali ilivyo sasa, ninaona kuna haja kuruhusu taasisi huru zije kutufanyia 'credit rating' ili itusaidie kama taifa kujua deni letu halisi likoje," Mdee alisema na kuongeza: "Kwa kutofanyiwa credit rating, benki nyingi za kimataifa zenye mikopo ya riba nafuu zitaendelea kuogopa kutukopesha kwa sababu hazina uhakika kama tutalipa au la. Matokeo yake tutaendelea kukopa kwa masharti magumu ya kibiashara.

"Sheria yenyewe ya Deni la Taifa imepitwa na wakati. Ni sheria ya miaka ya 1970. Hoja yetu hapa ni kwamba; tuwe na sheria inayoitaka serikali kukopa pale tu inapotaka kutekeleza miradi yenye uhakika wa kurejesha fedha na kulipa deni," alisema.

Wakati Mdee akishauri hayo, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, anaona kuna haja Bunge liunde kamati maalum ili kufanya ukaguzi wa Deni la Taifa.

Wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka 2019/20 bungeni jijini Dodoma Jumatatu iliyopita, Zitto alimwomba Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuunda kamati kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa deni hilo, akidai takwimu zinazotolewa hivi sasa si sahihi.

Kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo alisema usimamizi wa deni hilo ni tatizo, akiwataka wabunge kutazama ripoti za Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa miaka miwili iliyopita.

“Kwa sababu takwimu za sasa hivi siyo sahihi, mimi hapa nimesoma ripoti mbili za CAG; ya mwaka 2018 na ya mwaka 2019, inaonyesha kuna tatizo kubwa sana katika utunzaji wa kumbukumbu.

“Nakuomba Mheshimiwa Spika, uruhusu ukaguzi maalum ili tuweze kujua tunadaiwa nini na tunadaiwa na nani kwa sababu inawezekana kuna madeni hewa," Zitto alisema.