Ukraine yasisitiza umuhimu wa kupatiwa silaha za masafa marefu kwa ajili ya mashambulizi na ulinzi

FILE - Ukrainian President Volodymyr Zelenskyy attends a press conference in Kyiv, Ukraine, July 1, 2023.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy siku ya Ijumaa amesisitiza wito wake wa kupatiwa silaha za masafa marefu ili kufanya mashambulizi na operesheni za ulinzi dhidi ya majeshi ya Russia yaliyoivamia nchi yake.

Akizungumza Ijumaa wakati wa ziara yake huko Jamhuri ya Czech, Zelenskyy alisema Ukraine ilikuwa inazungumzia mifumo ya silaha za masafa marefu na washirika wengi, ikiwemo Marekani.

“Bila ya silaha za masafa marefu, siyo tu ni vigumu kufanya mashambulizi lakini pia, kiukweli, hata kujihami. Ni vigumu sana, Inamaanisha kuwa unaihami nchi yako na huwezi kufika masafa yanayostahiki kumuangamiza adui yako, hivyo, adui anakuwa na fursa ya kukushinda kwa sababu ya umbali aliyoko,” alisema.

Ziara ya Zelenskyy huko Prague ni sehemu ya ziara ya mataifa ya nje kabla ya mkutano wa NATO wiki ijayo, wakati ambapo anatarajiwa kuusihi muungano huo kuiingiza Ukraine kuwa mwanachama.

Umoja wa Ulaya ulisema Ijumaa kuwa wanachama wake wamefikia makubaliano kutumia dola milioni 545 kuimarisha uzalishaji wa silaha kwa ajili ya Ukraine na kujalizia silaha zilizotolewa na wanachama wake.